NA MARYAM SALUM, PEMBA

UONGOZI wa Hospitali ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, umewataka Jumuiya ya Vijana wa Kike, ‘Pemba Female Yourth Organization’ PFYO’ iliyopo Wete, kutochoka kujitolea kutoa ushirikiano kwenye maeneo ya kijamii, ili  kuhakikisha wanafikia malengo yao.

Katibu hospital hiyo, Hassan Kombo Hamad, aliyasema hayo wakati akizungumza na vijana wa jumuia hiyo, mara baada ya kumaliza kufanya usafi katika eneo la Hospitali hiyo, wakiwa   kwenye maadhimisho ya siku ya vijana duniani.

Alisema kuwa, uongozi wa Hospitali ya Micheweni pamoja na watendaji wake kiujumla, wamesema kwamba ujio huo umeonyesha mshikamano kati yao vijana hao na uongozi wa hospitali ya Micheweni.

Alisema kuwa furaha hiyo imekuja baada ya vijana hao wa kike kupamba moto wanakuwa na ushirikiano na taasisi nyengine pamoja na jamii kuhakikisha wanapambana na maisha kwa lengo la kuleta maendeleo ndani ya nchi.

 “Katika uongozi wangu ambao nimekaa hospitalini hapa sijawahi kuona jumuia hata moja ya kike, kuamua kufika kwenye maeneo yetu kutupa ushirikiano kama haya, kwakweli hawa ni vijana wenye mfano wa kipekee,” alisema.

Katibu huyo alifahamisha kuwa, kutokana ushirikiano huo kutoka kwa vijana hao, ni vyema na jumuia nyengine kujitolea kuonesha mfano kwenye  jamii kama ambavyo wamejitolea wenzao.

Aidha alifahamisha kuwa, Hospitali ya Micheweni ni moja ya hospitali ambazo zilikuwa nyuma kwa upande wa huduma na masuala mengine ya kiafya, lakini kutokana na juhudi za Serikali kujali wananchi wake, hospitali imeboreshwa na kua ya kisasa.