NAIROBI,KENYA                

KINARA  wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amewahimiza maseneta kuzingatia katiba ya mwaka 2010 katika ugavi wa mapato inayohimiza kuwepo kwa usawa katika ugavi wa rasilimali.

Kwa mujibu wa Kalonzo, maseneta wanapaswa kujua juhudi za Spika wa Seneti Ken Lusaka za kufanya mazungumzo ya jinsi ya kupata mwafaka wa mswada huo tata ambao mjadala wake uliahirishwa kwa mara ya saba sasa katika seneti.

Kinyume na msimamo wake wa awali, Kalonzo alisema usawa katika ugavi wa mapato ndio njia pekee itakayohakikisha kwamba taifa hilo linasonga mbele kimaendeleo.

Wakati huo huo alisema kuna haja ya mgao wa hazina ya mfuko wa usawa kuongezwa ili kuzisaidia kaunti nyengine ambazo zinakumbwa na changamoto ikiwemo ukame, zinazopata fedha za ziada za kuendesha shughuli zao.

Kauli ya Kalonzo ilikuja baada ya Kinara wa ODM Raila Odinga naye kubadili msimamo wake kuhusu mswada huo tata ambao hadi sasa, uligawanya bunge la seneti katika makundi mawili.

Naibu wa Rais William Ruto alikuwa miongoni mwa vigogo wa kwanza kupendekeza kutumika kwa mfumo wa awali ili kuhakikisha kwamba kila kaunti inanufaika.

Mkutano wa kutafuta mwafaka baina ya makundi hayo zilikosa kuzaa matunda baada ya maseneta wa upande wanaopinga mswada huo kukosa kutuma wawakilishi wao.