RAJAB MKASABA, IKULU

KIKAO cha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi kilichokaa jana chini ya Mwenyekiti wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, kimezipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia, ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, nae alihudhuria kikao hicho.

Katika taarifa ya umma kuhusu kikao hicho iliyotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole ilieleza kuwa miongoni mwa mafanikio hayo ni utekelezaji mzuri wa dira ya taifa ya mwaka 2020/2025, mwelekeo wa sera za CCM kwa miaka ya 2010-2020, Ilani ya CCM ya 2015-2020 pamoja na usimamizi madhubuti wa sera za kiuchumi nchini.

Kufuatia mafanikio hayo kwa kauli moja Kamati Kuu imeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mafanikio hayo.

Aidha, taarifa hiyo Kamati Kuu ilikaa jana ikiwa na lengo la kuandaa ajenda ya kikao cha halmashauri kuu ya Taifa ya CCM.

Kwa mujibu wa Polepole Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM itakutana leo makao makuu ya CCM Mjini Dodoma.