NA TATU MAKAME
KAMISHENI ya Utalii Zanzibar (ZTC) imesema imejipanga kushindana na mataifa mengine yanayofanya biashara ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini.
Mkurugenzi masoko wa kamisheni hiyo, Miraji Ukuti Ussi alieleza hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, ofisini kwake Amani mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Alisema nchi mbalimbali zimeanza kupokea watalii baada ya kupungua kwa ugonjwa wa corona duniani uliopelekea kusita kwa shughuli za kitalii kwa kipindi cha zaidi ya miezi 4.
Alisema wakati harakati hizo zimeanza zipo nchi zitakazofanya ushindani katika biashara hiyo, hivyo na Zanzibar haitokuwa nyuma katika mashindano hayo.
Alisema utalii ni miongoni mwa shughuli zinazoongeza mnyororo wa thamani kwa kuwa shughuli nyingi zinategemea utalii na kukosekana kwa utalii mambo mengi yalishuka na kupelekea uchumi kuterereka na nchi kushindwa kupokea watalii.
“Wakati janga la corona liliposhamiri nchi nyingi zilifunga mipaka na kusitisha safari za ndege lakini sasa harakati hizo zimerudi na sisi tupo tayari kushindana na mataifa mengine kuwavutia watalii kuja nchini,” alisema Mkurugenzi huyo.
Akizungumzia njia watakazozitumia kuona mikakati hiyo inatekelezwa, alisema kamisheni inaendelea na njia za kutangaza utalii ikiwemo mikutano kupitia njia ya mikutano ya mtandaoni (zoom meeting), kutumia vyombo vya habari na njia nyengine za mawasiliano ili kuhakikisha azma hiyo inafikiwa.
Akizungumzia uingiaji wa wageni katika kipindi cha Januari hadi Julai mwaka huu, alisema watalii 141,854 waliingia nchini wakati katika mwaka 2019 katika kipindi kama hicho watalii 235,020 walitembelea Zanzibar.
Nae Mwenyekiti Kamisheni hiyo, Sabahi Saleh Ali alisema katika kuhakikisha lengo linafikiwa wanaendelea kutoa elimu kwa watembeza wageni na wadau wengine kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi hayo.
“Pamoja na kurudi kwa shughuli, bado tunawataka watu wote wanaojihusisha na biashara ya utalii na watalii wenyewe wandelee kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa corona pale wanapokuwa kazini,” alisistiza mwenyekiti huyo.
Hata hivyo alisema elimu hiyo pia waliitoa kwa wanawake wa vijijini wanaojihusisha na biashara ya utalii ili na wao wapate kuendelea na kazi zao bila ya madhara.
Sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa fedha za kigeni nchini ambayo kutokana na kuzuka kwa maradhi ya covid 19, iliporomoka hasa baada ya nchi nyingi kusitisha safari za ndege za kimataifa ikiwemo Zanzibar.