MOJA ya sifa njema iliyonayo nchi yetu inayozungumzwa nje kwa fahari kubwa, ni suala la amani, na umoja wetu tulionao, ambao kwa hakika serikali zetu mbili zinachukua jitihada kubwa kuhakikisha tunu hizo zinadumu daima.
Tunapozuungumzia umoja katika muktadha huu tunaamanisha ni ile hali ya wananchi kujifaharisha na kujivunia kwa uzalendo mkubwa kwao wao ni watanzania, bila ya kujali ukabila, udini, rangi ya mtu nakadhalika.
Na tunapozungumzia amani tunaamanisha ni ile hali ya mwananchi wa kawaida kufanya shughuli zake za kimaisha, kiimani na kimaendeleo bila ya bughdha ama hofu ya maisha yake.
Hivi tunavyozungumza hapa duniani zilikuwepo nchi kadhaa ambazo zilidumu kwenye umoja na amani, lakini kwa bahati mbaya sana baada ya kukubali chokochoko na kuchezea kwa amani na utulivu walionao mambo yamegeuka.
Katika nchi hizo imefikia hatua mwananchi mmoja anamvizia mwengine akiwa na silaha za jadi na wengine watwangana risasi, wananchi katika nchi hizo wamejawa hofu kiasi cha kutokuwa na uhakika wa kesho yao itakuwaje.
Sio kwamba katika nchi hizo hakuna jitihada zinazochukuliwa za kuirejesha amani na utulivu, vikao vya kimikakati vinajadili namna ya kuirejesha amani, lakini kumekuwa na ugumu mkubwa hali inayosadifu msemo wa kiswahili maji yakimwagika hayazoleki.
Haya yanayotokea katika nchi za wenzetu ambayo wakati mwengine yanaonekana kama mchezo wa sinema, kama wazanzibari tukiyatafakari bila ya kutumia akili kubwa bila shaka tutabaini yapo mengi ya kujifunza.
Amani na utulivu uliopo Tanzania na Zanzibar tunadiriki kusema kuwa ni miongoni mwa tunu zetu muhimu, hivyo hatupaswi kuzichezea ama kujaribu kuziweka rehani kwa kuwafumbia macho wale wanaotia chokochoko ya kuziharibu tunu hizo.
Tunalazimika kuyasema haya wakati huu ambapo Tume za Uchaguzi Tanzania tayari zimefungua mapazia ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Uzoefu unaonesha kuwa katika kipindi kama hichi wapo watu ama vikundi vya watu wenye dhamira na malengo ya kujaribu kuchezea amani, umoja na utulivu wetu kwa maslahi yao, hili ni jambo la hatari sana.
Watu wa namna hiyo, mara nyingi hutumia visingizio vya siasa katika kuihujumu na kuijeruhi amani na utulivu wetu, roho zao huwa burudani pale wanapoona amani inachafuka watu wanakufa, akina mama na watoto wanaishi kwa dhiki wengine wako kwenye kambi za wakimbizi.