Wananchi wanalizungumziaje jembe hilo la CCM?

NA MWANDISHI WETU

“WAPO wanaosema kwamba mimi mpole sana, lakini nimejifunza kutoka kwako (Rais Magufuli) kwamba kuna mambo ya msingi; rushwa, uzembe na ubadhirifu yanataka uwe mkali na hilo nataka niwaahidi wananchi kwamba endapo nitachaguliwa kuwa rais, wategemee nitakuja na staili ya rais Magufuli katika maeneo hayo.”

Hii ni kauli ya kwanza ya mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Mwinyi, baada ya kushinda kwa kura 129 katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, uliofanyika Dodoma Julai 11 mwaka huu.

Wakati anaingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, Rais Magufuli aliahidi kupambana na rushwa na muda mfupi akaanza kutekeleza ahadi hiyo kwa kuwashughulikia watu waliokuwa wakituhumiwa kwa rushwa huku akianzisha mahakama maalum ya kukabiliana na ufisadi.

Mapambano dhidi ya rushwa sio tu yalimpaisha Dk. Magufuli na kuonekana kuwa kiongozi wa mfano katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Kusini mwa Jangwa la Sahara, lakini pia yalijenga nidhamu kubwa katika taasisi za umma.

Hii ndio staili ambayo mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM anataka kuiga kama atachaguliwa na wananchi katika uchaguzi wa mwezi Oktoba.

Dk. Mwinyi sio mgombea wa kwanza katika historia ya uchaguzi wa vyama vingi Zanzibar kutoa kauli kama hii. Wapo wengi kama sio wote walitoa ahadi ya kudhibiti rushwa pindi watakapoingia madarakani.

Hata hivyo, matokeo yake rushwa imekuwa sehemu ya maisha ya wananchi kwa sababu hatua zilizochukuliwa za kukabiliana na uovu huu hazijatosha kumaliza tatizo hilo na kama zilichukuliwa hazikuwekwa wazi kiasi kwamba wananchi hawakuwa na taarifa na kile kilichofanywa.

Wananchi wamejenga matumaini na ahadi ya mgombea huyu ambae amefanya kazi kwa miaka mitano chini ya Dk. Magufuli na pia kuhudumu katika serikali za awamu nyengine mbili za muungano ya awamu ya tatu  iliyoongozwa na Benjamin Mkapa na ya nne chini ya Jakaya Kikwete.

Fatma Sadiki (46) mkaazi wa Mtoni wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, anasema ahadi ya Dk. Mwinyi ya kupambana na rushwa na ubadhirifu imemsisimua na kujenga matumaini mapya ya kuviona visiwa vya Unguja na Pemba vikinawiri upya.

“Nitakwenda kumpigia kura ili nimpe nafasi ya kukabiliana na rushwa, tumechoka. Unanyimwa haki yako ya msingi kwa sababu tu hujatoa rushwa, inaonekana maisha bila rushwa hayawezekani tena,” alisema Fatma.

Kwa Fatma, rushwa imechukua nafasi kubwa na wakati mwengine kusababisha migogoro ya kifamilia.

 “Wakati mwengine unapokua na mume mfanyakazi ambae anaichukia rushwa unamshangaa, kwanini aache kuchukua rushwa wakati wengine ndio utamaduni wao?” alihoji Fatma mama wa watoto watano.

Ingawa anakiri kwamba serikali ya awamu ya saba imechukua hatua mbali mbali madhubuti kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuanzisha Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA).

Hata hivyo, anasema bado kuna safari ndefu ya mafaniko hadi kuaminiwa na wananchi kama ilivyo kwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (TAKUKURU), ambayo tokea ianzishwe imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 273.3.

Mussa Mbarouk (55) mkaazi wa Bububu Kijichi, hana shaka na uwezo wa Dk. Mwinyi wa kutokomeza ushwa lakini kwake kazi hiyo itakuwa rahisi sana iwapo Dk. Mwinyi ataiimarisha ZAECA ili iwe na uwezo wa kusimamia kesi mahakamani kama ilivyo TAKUKURU.

“Kuna haja kwa Dk. Mwinyi kama ataingia madarakani kuiimarisha ZAECA kwa sababu uwezo wake wa kukabiliana na rushwa kubwa bado mdogo, lakini naamini kwa sababu amejifunza kutoka kwa Rais Magufuli ataweza kuifanya kazi hii kwa ufanisi. ZAECA ni muhimu, hatuwezi kuzungumzia uchumi wa viwanda kama hatujaimarisha taasisi hii,” alisema.

Mussa sio pekee alieguswa na ahadi ya Dk. Mwinyi ya kukabili ufisadi. Muhusini Ramadhani (27) wa Masingini Mwera, anaamini kwamba Zanzibar inaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo kama kutakuwa na juhudi za dhati na za wazi katika kukabiliana na tatizo hilo.

“Anatakiwa kutowaonea aibu wala muhali watu wanaopokea rushwa hata kama ni marafiki zake, hii ndio staili ya Rais Magufuli. Aliwaandama wale ambao tuliamini hawawezi kuguswa kutokana na nafasi zao katika jamii au serikalini. Kasi kama ya Magufuli ndio anatakiwa kuanza nayo,” alisema.

Muhusini anasema mwanzoni hakuamini kama Rais Magufuli angeweza kudhibiti rushwa na watu wengi waliona ni mzaha tu kwa sababu waliamini Tanzania isiyo na rushwa haiwezekani, lakini leo amekuwa mfano wa kuigwa na Marais wengine wa Afrika.

Ali Shaali (29) wa Shaurimoyo wilaya ya Mjini Unguja, nae amewaka bayana kwamba atamchagua Dk. Mwinyi baada ya kujipambanua kwamba atakabiliana na rushwa, uzembe na ubadhirifu wa mali za umma.

“Sikupiga kura katika uchaguzi uliopita (2015), lakini mwaka huu nitapiga kura na niweke wazi kwamba nitamchagua Dk. Mwinyi kutokana na msimamo wake wa kukabili rushwa si vyenginevyo. Rushwa imetuchosha, kila kitu hata kama ni haki yako kupewa bila malipo kwanza unadaiwa kitu kidogo,” alisema.

Safinia Masoud (35) wa Kwamtipura, anafikiria ili rushwa iweze kupungua katika jamii lazima urasimu katika upatikanaji wa haki za msingi upunguzwe.

“Mara nyengine watu hawataki kutoa rushwa, lakini urasimu na upatikanaji wa huduma kuchukua muda mrefu inasababisha washawishike kutoa rushwa wakiamini kufanya hivyo itasaidia kupata huduma kwa wakati na kwa urahisi. Hivyo Dk. Mwinyi kama atachaguliwa lazima akabiliane na urasimu kwanza kabla ya kutokomeza rushwa”, alisema.

Pia anasema kuna haja kwa ZAECA kujengewa uwezo wa kufanya uchunguzi, uwezo wa wafanyakazi ikiwemo maslahi bora ili kupunguza ushawishi wa kupokea rushwa kutoka kwa wanaochunguzwa na uwezo wa kielimu.

“Taasisi hii ni muhimu katika mapambano haya, hivyo lazima ijengewe uwezo wa hali ya juu vyengine itaendelea kushughulikia rushwa ndogo huku wala rushwa wakubwa wakiachw kuendelea kuwa wafalme”, alisema.

Mbali ya rushwa, Dk. Mwinyi ameahidi kukabiliana na ubadhirifu wa mali za umma na uzembe.

Ridhiwani Massoud (40) wa Amani Mkoa wa Mjini Magharibi, anasema ingawa serikali ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kudhibiti ubadhirifu wa mali za umma na uzembe kwa kupunguza tabia ya kufanya kazi kwa mazoea kwa watumishi wa umma, bado kuna safari ndefu kufikia mafanikio ya kujivunia.

“Dk. Shein amefanikiwa kuunda mamlaka ya ununuzi wa mali za umma ambayo imeanza kazi vizuri kudhibiti matumizi holela ya fedha za umma kwenye manunuzi, lakini bado zipo changamoto ambazo tunaamini Dk. Mwinyi kama atachaguliwa anapaswa kuzikabili kwa nguvu zote ikiwemo uwezo wa taasisi yenyewe kwa sababu ya uchanga wake,” alisema.

“Wakati mwengine unakuta miradi inajengwa lakini baada ya muda mfupi pengine miezi mitatu tu inaharibika, huu ni ubadhirifu wa mali za umma ambao unastahiki kuchukuliwa hatua kali.

Aidha, anasema Dk. Mwinyi kama atachaguliwa ahakikishe ujenzi wa miradi ya maendeleo unalingana na thamani ya fedha kama anavyofanya Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk. Shein.

“Rais Magufuli amefanikiwa kusimamia nidhamu katika matumizi ya fedha za umma katika ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa kuhakikisha mradi unalingana na thamani ya fedha zilizotolewa. Tumeshuhudia watendaji wengi wakipoteza ajira zao kwa sababu ya nidhamu mbovu katika matumizi ya fedha za umma kwenye miradi ya maendeleo. Tunaamini Dk. Mwinyi atalisimamia hilo,” alisema Mwinyi Zubeir (46) wa Fuoni.

“Juzi wakati anafungua makao makuu ya TAKUKURU Dodoma alihoji maombi ya shilingi bilioni moja kwa ujenzi wa ukuta wakati alitoa fedha kama hizo kwa ujenzi wa ofisi za serikali. Amebaini shilingi bilioni moja alizoombwa ni nyingi na haziendani na thamani ya mradi unaotaka kujengwa,” alisema.

Lakini pia anasema, Rais Magufuli alihoji kuhusu ujenzi wa ofisi yengine ya chini iliyojengwa kwa shilingi milioni 140 na kuonya kwamba kama atafanikisha kujenga jengo kama hilo kwa thamani ya shilingi milioni 60, basi bosi wa TAKUKURU na wasaidizi wake wajiandae kung’oka.

“Naamini Dk. Mwinyi atakuwa mkali kama ilivyo kwa mtu anaetaka kuiga staili yake ya uongozi kwa sababu waswahili wanasema ‘mrithi huzidi’,” alisema Zubeir.