JUMANNE ya Agosti 18 ndiyo siku ambayo wanajeshi nchini Mali walimuondosha marakani rais wa nchi hiyo aliyechaguliwa kidemokrasia, Ibrahim Boubacar Keita.
Wiki moja kabla ya Keita kuondolewa ikulu, taarifa zilieleza kuwa zilikuwepo ishara za kutokea kwa mapinduzi hayo, kufuatia baadhi ya wanajeshi kufyatuliana risasi mjini Bamako.
Pamoja na kwamba jumuiya za kimataifa kuyalaani mapinduzi yaliyomuondoa madarakani rais Keita na kutaka kutaka kurejeshwa kwenye kiti rais hiyo, maofisa wa jeshi wanaonekana hawana dhamira hiyo kwa sasa.
Hivi sasa maofisa wa jeshi wanapanga namna ya kuunda serikali ambayo itakuwa na mchanganyiko baina ya wanajeshi na rais wa nchi hiyo, ikiitwa serikali ya mpito kuelekea kwenye maandalizi ya uchaguzi mkuu.
Kuonesha kughadhibishwa na mapinduzi hayo, ECOWAS jumuiya ya maendeleo ya kiuchumi kwa nchi za magharibi ya Afrika, imetuma ujumbe maalum kuzungumza na wanajeshi ili wafute mapinduzi waliyoyatekeleza.
“Wakati wa mapinduzi umekwisha”, imekumbusha jumuiya ya ECOWAS na huu ni ujumbe ambao imekusudia kuufikisha kwa kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi.
ECOWAS imechukuwa hatua za kuzuia uingiaji wa fedha na shughuli mbalimbali za kiuchumi pia zimesitishwa, isipokuwa dawa, mafuta na umeme kwa ajili ya mahitaji ya waanchi wa Mali.
“Nadhani vikwazo hivi vilivyoekwa na ECOWAS ni vikali. Na ninaelewa kabisa kuwa ECOWAS imechukuwa maamuzi kwa misingi wa mikataba na itifaki zake”, alisema Moussa Mara, waziri mkuu wa zamani wa Mali.
Mwezi mmoja baada ya kuchaguliwa na kuwa rais wa Mali mnamo 2013, Ibrahim Boubacar Keita alitangaza kwamba siku za wanajeshi wenye nia ya kudhoofisha nguvu ya serikali zimefika mwisho wake.
Kiongozi huyo alisema hayo huku akitolea mfano kambi ya kijeshi ya Kati iliyopo nje ya mji mkuu ambapo uasi uliopita ulisababisha kuondolewa madarakani rais wa wakati huo Amadou Toumani Toure.
Kwa bahati mbaya sana uasi wa jeshi ulioanza kambi hiyo hiyo ambayo iko umbali wa kilimomita 15 kutoka mji mkuu Bamako miaka saba baadaye, Keita, mwenye umri wa miaka 75, naye amejikuta kwenye hatima ile ile iliyomkuta mtangulizi wake.
Mapinduzi yaliyomg’oa madarakani Keita mnamo Agosti 18 mwaka huu, uasi wake ilianzia kwenye kambi ya Kati ambapo masaa machache, risasi zilisikika hewani huku waasi hao wakiendesha gari kuelekea mjini.
Walipofika Bamako waliingia ikulu na kumbeba rais na kumchukua hadi kwenye kambi ya kati ambapo alilazimishwa ajiuzulu na pia kulivunja bunge la nchi hiyo. Kwa upole kabisa Keita akaachia ngazi.
Licha ya ahadi kemkem alizozitoa kwa wananchi wa Mali ikiwemo kumaliza matatizo ambayo yalisababisha kung’olewa madarakani mtangulizi wake, lakini Keita inaonekana alishindwa kuyatatua matatizo hayo.
Miongoni mwa changamoto ambazo mtangulizi wake zilisababisha aondoke madarakani na ndiyo hizo hizo zilizomuondoa madarakani Keita, ikiwemo matatizo ya usalama yanayosababishwa na makundi ya waasi wa kaskazini mwa Mali.
Aidha jamii kubwa ya wananchi wa Mali wanalalamika kuwepo kwa tatizo la kukithiri kwa rushwa, Keita alishindwa kabisa na hivyo kujikuta wapinzani wakifanya maandamano.
Mgogoro wa uchaguzi wa bunge uliofanyika mnamo mwezi Aprili na uchumi uliosambaratika vilizidisha hasira za raia wa Mali, hali ambayo iliwafanya maelfu ya watu kuandamana katika mitaa ya mjini Bamako katika wiki za hivi karibuni waliomtaka kiongozi huyo ajiuzulu.
Keita, maarufu sana kwa kuitwa kutokana na herufi za kwanza za majina yake IBK, alishinda uchaguzi wa marudio miaka miwili iliyopita na serikali yake ya muungano ilikuwa na uungwaji mkono mkubwa bungeni.
Ibrahim Maiga, mtafiti wa nchini Mali kutoka kwenye taasisi ya masomo ya usalama alissema rais Keita hakuelewa haraka hasira iliyokuwepo miongoni mwa jamii nzima.
Maiga alisema kiongozi huyo hakuzisoma alama za nyakati kwamba kulikuwepo na mahitaji makubwa ya mabadiliko nchini humo jambo lililochangia kung’oka madarakani.
Keita aliingia madarakani akiwa na sifa ya kuwa mtu aliyekuwa sio mwepesi kutingishwa kwa kuzingatia enzi alipokuwa waziri mkuu katika miaka ya 90 wakati alipochukua maamuzi magumu dhidi ya waliounga mkono na waandaaji wa mgomo wa vyama vya wafanyikazi.
Lakini tangu mwanzo hakuweza kupata suluhisho la kuushughulikia mgogoro uliotishia usalama wa Mali kaskazini mwa nchi hiyo.
Vikosi vya Ufaransa viliingilia kati mnamo Januari 2013 na kuwarudisha nyuma wapiganaji wenye misimamo mikali wanaohusiana na kundi la kigadi al Qaeda ambao walitumia uasi wa kabila la Tuareg na wakafaulu kudhibiti theluthi mbili ya eneo la kaskazini mwa nchi.
Serikali ya rais Keita ilikuwa inapambana kuwadhibiti wanamgambo wa Tuareg waliokuwa wanataka kujitenga.
Keita aliungwa mkono sana na jamii ya kimataifa, haswa kutoka kwa mkoloni wa Mali wa zamani Ufaransa, nchi ambayo ilimwaga pesa nyingi nchini humo pamoja na na askari.
Lakini serikali Keita yake ilijikuta inakabiliwa na lawama na madai ya ulaghai kuhusiana na ununuzi wa ndege ya rais iliyogharimu dola milioni 40 na matumizi mabaya katika ununuzi wa vifaa vya jeshi hatua iliyosababisha Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kuchelewesha misaada kwa muda.
Ahmedou Ould-Abdallah, mwanadiplomasia wa Mauritania na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa katika Afrika Magharibi alisema wakati ambapo kuna uwepo mkubwa wa jeshi la nje, fursa za ufisadi nazo huwa kubwa.
Mwanawe rais Keita, Karim Keita anakabiliwa na lawama za kuhusika na ufujaji fedha za umma kutokana na jinsi anavyoishi maisha ya juu na vyeo alivyonavyo ikiwa ni pamoja na kuwa mwenyekiti wa kamati za bunge za ulinzi na usalama.
Katika runinga msemaji wa kundi lililomg’oa Keita madarakani alikosoa nguvu za kisiasa na usimamizi wa mambo ya serikali zilizokuwa chini ya familia ya Keita.
Msemaji huyo wa umoja wa M5-RFP Nouhoum Togo alieleza kwamba, IBK, yaani Ibrahim Boubacar Keita hakutaka kuwasilikiza watu wake ndipo maandamano dhidi yake yalipoanza na yeye kwamba Ufaransa au jamii ya kimataifa itamuokoa.