NAIROBI,KENYA

SHIRIKA  la Nishati ya Nyuklia la Kenya (NUPEA) limewasilisha ripoti kuhusu mpango wa ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa nyuklia ambacho ujenzi wake unatarajiwa kugharimu dola bilioni tano.

Kwa mujibu wa tovuti ya Bloomberg, ujenzi wa kituo hicho unakaribia kuanza na kitazinduliwa katika kipindi cha miaka saba ijayo.

Shirika la Nishati ya Nyuklia la Kenya limewaswilisha ripoti ya ujenzi huo kwa Shirika la Kitaifa la Usimamizi wa mazingira kenya (NEMA), huku ripoti zikisema Serikali ya Kenya inapanga kuzalisha megawati 4,000 za nishati ya nyuklia ifikapo mwaka 2035.

Baada ya NUPEA kuwasilisha ripoti hiyo kwa NEMA, wananchi wa Kenya wanatarajiwa kujadili masuala ya kimazingira yanayohusiana na ujenzi wa kituo hicho cha nyuklia.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alitangaza azma ya kuhakikisha kuwa uzalishaji umeme wa Kenya unaimarishwa kutoka megawati 2,712 hivi sasa hadi megawati 22,000 ifikapo mwaka 2031 ili kuimarisha sekta ya viwanda katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi mashariki mwa Afrika.

Kituo hicho cha nyuklia nchini Kenya kinatarajiwa kujengwa katika Kaunti ya Tana River iliyo katika eneo la pwani.