NAIROBI, KENYA

HARAKATI  ya Mshikamano wa Kenya na Palestina imelaani vikali mapatano yaliyofikiwa baina ya watawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu za utawala ghasibu wa Israel chini ya usimamizi wa makundi ya Israel nchini Marekani.

Katika taarifa yake Katibu wa Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina Kenne Mwikya alisema,baada ya miaka mingi ya uhusiano wa siri baina ya tawala za Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu, pande mbili zilifikia mapatano ambayo yatapelekea kuanzishwa uhusiano chini ya usimamizi wa Serikali ya Trump.

Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina ilisema mapatano hayo yatatumika kuimarisha utawala wa Israel ambao unakalia ardhi za Palestina kwa mabavu sambamba na kuwapa nguvu watawala wa Kiarabu ambao wanatekeleza jinai dhidi ya watu wa Yemen, Libya, Syria na Iraq.

Kufuatia hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa lengo la kurahisisha uanzishwaji uhusiano wa kawaida kati ya UAE na Israel,pande hizo mbili za Abu Dhabi na Tel Aviv zilisaini mkataba na kuafikiana rasmi kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia.

Taarifa ya Harakati ya Mashikamano wa Kenya na Palestina ilisema mapatano hayo si kwa maslahi ya watu wa eneo bali ni kwa maslahi ya tawala hizo mbili.

Kenne Mwikya alisema harakati ya mashikamano wa Kenya na Palestina inajiunga na Wapalestina kuwalaani viongozi wa UAE ambao wamewasaliti Wapalestina katika mapambano yao ya uhuru.

Hata hivyo harakati ya Mashikamano wa Kenya na Palestina ilitoa wito wa kususiwa Umoja wa Falme za Kiarabu hasa matamasha ya kiutamaduni,kicuhumi na kimichezo ambayo hufanyika katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Taarifa hiyo aidha ilisisitiza kuhusu kususiwa safari zote kuelekea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).