NA TATU MAKAME

KESI ya kumuingilia kimwili mtoto wa kike inayomkabili mtoto wa miaka 16 mkaazi wa Magomeni Wilaya ya Mjini Unguja, imeahirishwa katika mahakama ya Mkoa Vuga hadi Septemba 1 mwaka huu kwa kusikilizwa.

Kesi hiyo imeahirishwa na Hakimu Valentine Andrew Katema wa mahakama ya mkoa Vuga, baada ya mshitakiwa huyo kukana shitaka hilo mara baada ya kusomewa mahakamani hapo.

Shitaka hilo alisomewa na Mwendesha Mashitaka Ahmed Mohammed, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Katika shitaka hilo, mshitakiwa huyo alidaiwa kutenda kosa la kumuingilia kimwili mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 (jina linahifadhiwa).

Kosa hilo ni kinyume na vifungu vya 125 (1) (2) (e) na 126 (2) vya sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar, tukio ambalo alidaiwa kulitenda Disemba 17, 2017 majira ya saa 10:00 za jioni.