Addis Ababa, Ethiopia
KIPA wa zamani wa Simba, Daniel Agyei ameiponza timu ya Jimma Abar Jifar ya Ethiopia baada ya klabu hiyo, inayoshiriki Ligi Kuu ya Ethiopia kufungiwa usajili katika madirisha matatu kutokana na kutomlipa stahiki zake.
Kamati ya usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), juzi Agosti 11 iliamua kuwa klabu hiyo, inatakiwa kumlipa Agyei, madai yake yote adhabu ambayo itaambatana na kifungo cha kutosajili kwa madirisha matatu mfululizo.
Katika usikilizaji na usuluhishi wa shauri hilo lililofunguliwa na Agyei tangu Aprili 15 mwaka huu, kamati hiyo ya usuluhishi ya FIFA, imegundua kuwa klabu hiyo ya Jimma Abar Jiffar imekiuka makubaliano ya kimkataba baina yao na kipa huyo, jambo ambalo ni kinyume na muongozo wa hadhi za wachezaji.
Kwa mujibu wa uamuzi huo uliotolewa na FIFA, Klabu hiyo ya Ethiopia imetakiwa kuhakikisha inalipa stahiki za Agyei, ndani ya muda mfupi tangu adhabu hiyo ilipotangazwa na kama ikishindikana kamati hiyo itaongeza adhabu zaidi kwa klabu hiyo.
Agyei alijiunga na Jimma Abar Jifar mwaka 2017 akitokea Simba ambayo ilimsajili mwaka 2016 kutokea klabu ya Medeama ya Ghana.