LONDON, England
NAHODHA wa Manchester United, Harry Maguire, ameonyesha kukasirishwa na kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Europa kwa kuchapwa na Sevilla CF magoli 2-1.

United iliandika goli la kuongoza kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Bruno Fernandez kunako dakika ya tisa kabla ya Sevilla kusawazisha kupitia kwa Sergio Reguilon, huku Luuk de Jong akifunga goli la ushindi katika dakika ya 78.

Hata hivyo, mlinda mlango wa Sevilla CF, Bounou alipaswa kupewa sifa kubwa kwa kazi nzuri aliyoionyesha wakati wote wa pambano hilo kwa kuzuia nafasi kadhaa za mabao.
Akizungumza na BT Sports baada ya mchezo huo, Maguire, alisema: “Kufungwa hakukubaliki. Kuishia hatua ya nusu fainali hakukubaliki. Kushinda mataji kunakaribia, tunahitaji kushinda mataji”.

“Timu bora imefungwa, wametuhukumu kwa nafasi tulizokosa. Tumefungwa kwa kona mbili kitu ambacho sio sahihi.

” Tulicheza vizuri na kustahili ushindi, tumeishia hatua ya nusu fainali kwa mara ya tatu msimu huu. Pengine ukosefu wetu wa uzoefu umetugharimu, tusingefungwa zile kona mbili”.

Naye Meneja wa United, Ole Gunnar Solskjaer alisema: “Inahuzunisha, ni ngumu kukubali. Tumecheza vizuri na kutengeneza nafasi, lakini, hatukupata matokeo tuliyoyahitaji”.

“Tunahitaji kuimarisha kikosi chetu, siwezi kusema lini au kama tutasajili, lakini, tunaliangalia hilo. Tunapaswa kuwa na uhakika wa asilimia 100% katika kutekeleza hilo”.

Kwa kupoteza nafasi ya kucheza fainali ya Ligi ya Europa msimu huu, sasa ni rasmi United wanamaliza msimu wakiwa wamecheza nusu fainali tatu bila ya ushindi.
Katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, United walimaliza katika nafasi ya tatu, pointi 33 nyuma ya mabingwa Liverpool.(Goal).