NA KHAMISUU ABDALLAH

WAZIRI wa Fedha na Mipango Zanzibar, Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa, amesema kuanza kazi kiwanda cha kuzalisha nguo cha Basra kutatoa fursa ya ajira kwa vijana wa Zanzibar.

Balozi Ramia aliyasema hayo wakati alipofanya ziara katika kiwanda hicho kilichopo Chumbuni ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kuangalia maeneo ya kiuchumi.

Aidha, alisema kiwanda hicho kwa hatua ya kwanza kitatoa ajira kwa wazalendo 453 na baadae vijana 1,200 na miezi 18 inayokuja itatoa ajira za watu 1,600 hivyo ni vyema kuitumia fursa hiyo ili kuondokana na utegemezi katika familia zao.

“Ikiwa vijana wetu wataitumia fursa hii vizuri kwa kuomba ajira pale zinapotangazwa basi wataweza kusaidiana na wawekezaji hawa katika kukiendeleza kiwanda chetu kiwe kinafanya kazi kwa urahisi,” alisema.

Alisema uwepo wa viwanda hivyo nchini vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa nchi na kusaidia serikali katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Balozi Ramia, alibainisha kuwa serikali imeona mradi huo una manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi hivyo aliwaomba wananchi wa maeneo hayo kushirikiana na wawezekaji hao kuhakikisha wanatunza eneo hilo na kuona hakuna uharibifu unaojitokeza.

“Wananchi wawasaidie wawekezaji hawa kuona wanafanya kazi kwa amani na kuona manufaa yanayopatikana katika kiwanda hichi basi ni manufaa kwa wananchi wote kwa ujumla,” alisisitiza.

Alisema, serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji hao katika kila hatua ili kuona kiwanda hicho kinaanza kazi na wananchi wananufaika na bidhaa wanazozalisha na vinawafikia.

“Mchango wa serikali ni mkubwa kwa kiwanda hichi kuona mashine zinazoletwa na malighafi basi ushuru wake hauwi mkubwa ili kukiwezesha kuzalisha bidhaa zenye gharama nafuu na wananchi wetu wanamudu kuzinunua,” alisema.

Hivyo, aliwaomba wawekezaji hao kuhakikisha wanawafundisha vijana wazalendo kazi zitakapoanza ili kuondokana na utamaduni wa kuwaita watu kutoka nje ya nchi.

“Lengo letu kuona mnawafundisha vijana wetu wazalendo, hatupendi kuona mara kwa mara mnawaita watu kutoka nje tunataka vijana wapate ujuzi wa kuweza kufanya kazi mbalimbali ambazo zitawawezesha kujiajiri na kujikwamua na umasikini,” alisisitiza.

Kwa upande wake Meneja Operesheni wa Kampuni hiyo, Ali Idrissa alisema kiwanda hicho kitakapoanza kazi basi kitazalisha sare za skuli, vitenge, vitambaa na bidhaa nyengine za nguo.

Aidha alisema baada ya miezi 18 wanatarajia kuingiza charahani 500 ambazo zitatumika kwa ajili ya kushona madira ya kike, shati za kiume, fulana na nguo nyengine ambapo wananchi watanunua bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.  

Alitumia muda huo kuipongeza serikali kutoa msaada mkubwa kwa wawekezaji hao na kuahidi kuendelea kushirikiana ili kuona lengo lililokusudiwa linafikiwa.

Aliahidi kuwa kiwanda hicho kitaajiri vijana wazawa ili kuona wanafundishwa kazi ambazo zitapelekea kupata ujuzi.

Kiwanda hicho kinatarajia kuanza kazi Oktoba mwaka huu ambapo kwa hatua ya kwanza mradi huo umegharimu dolla za Marekani millioni 23 ikiwemo ununuzi wa mashine.