ZASPOTI
KOCHA mkongwe wa soka visiwani hapa, Salum Masoud Salum ‘Masoud Kocha’, anatarajiwa kuanzisha akademia ya michezo mbali mbali kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo nchini.
Akizungumza na Zaspoti, Kocha huyo, alisema, akademia hiyo inatarajiwa kuanza rasmi mwezi Septemba mara taratibu za usajili zitakopomalizika.

Alisema, akademia hiyo itakayojulikana kwa jina la ‘Small Simba Sports Academy’ itakuwa ikifundisha michezo mbali mbali ikiwemo mpira wa kikapu, pete, meza, magongo, gofu, kriket, skwashi na mchezo mkuu wa soka.

“Mpaka hivi sasa tayari tumeshapata wakufunzi wa michezo hiyo na tutafundisha bila ya malipo yoyote”, alisema.
Kocha huyo wa zamani wa Small Simba na timu ya vijana ya Zanzibar chini ya umri wa miaka 17, alisema, lengo la kuanzisha kwa chuo hicho ni kuinua michezo yote ambayo mengi yao imekufa ili vizazi vijavyo viweze kuijua.

Alisema elimu watakayoitoa itaanzia kwa watoto wenye kuanzia umri wa miaka 5-23 ambapo hadi hivi sasa wameshapata vijana 600 tayari kujifundisha michezo mbali mbali.
Hata hivyo, alisema, mbali na kutoa elimu katika chuo hicho na kufanya mazoezi kwenye uwanja wa timu ya Small Simba, Maisara pia watazunguka katika mikoa mbali mbali ya Tanzania kutoka taaluma hiyo.

“Tunatarajia kuhakikisha elimu tutakayoitoa itawafikia vijana wote wa Tanzania kwani tumedhamiria kuzunguka mikoa mbali mbali kwa lengo la kustawisha michezo nchini”, alisema.
Masoud Kocha aliiomba serikali pamoja na wadau wa michezo kumpa ushirikiano katika kuhakikisha jambo hilo linafanyika na kurudisha michezo nchini.