NA TATU MAKAME

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano la kikao kazi cha kuboresha shughuli za utalii lililoandaliwa na wadau wa utalii litalofanyika Hoteli ya Verde iliyopo Mtoni kisiwani hapa.

Akizungumza na mwandishi wa habari Ofisini kwake Mlandege mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasambazaji na Waratibu wa shughuli za utalii (ZATO), Hassan Ali Mzee alisema kongamano hilo la siku mbili litaanza leo na kesho.

Alisema lengo la kuandaa kongamano ni kuendeleza utalii na kuboresha sekta hiyo hapa nchini.

Alisema kuwa kongamano hilo litawahusu wadau wote wanaohusika na shughuli za kitalii wakiwemo watembezaji na wadau wa utalii na zitazishirikisha taasisi mbalimbali za serikali na binafsi kutoa maoni yao ili yapate kufanyiwa kazi kwenye jumuiya.

Alisema mada mbalimbali zitawasilishwa ikiwa ni pamoja na soko la utalii (marketing), kuweka mifumo sawa ya uendeshaji wa shughuli za kitalii, Masuala ya covid 19 katika kipindi cha corona na athari zilizopatikana.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Sabah Saleh Ali alisema kufanyika kwa kongamano hilo kutasaidia kupeleka mbele shughuli za utalii pamoja na kutangaza vivutio vya ndani.