Wanahabari wasikubali kutumiwa vibaya na wanasiasa

Wakumbuke kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi

Na Ali Othman

KIPENGA cha kampeni ya kuelekea uchaguzi mkuu wa Tanzania tayari kimepigwa na kwamba baadhi ya maeneo tayari hapo jana kampeni zimeshaanza.

Baada ya pazia la urejeshwaji fomu za wagombea wa urais na ubunge kwa tume ya Taifa ya uchaguzi Tanzania bara na ubunge kwa Zanzibar kufungwa rasmi hapo juzi baada ya wabunge kurejesha fomu zao.

Aidha pazia kwa ajili ya urais wa Zanzibar kwa vyama mbalimbali kufunguliwa hapo jana na Tume ya uchaguzi Zanzibar, ambapo mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi.

Katika makala haya tunazungumzia namna ya wanahabari wanavyopaswa kufanya kazi zao katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi, siku ya uchaguzi, kutangazwa matokeo n ahata baada ya kupatikana mshindi wa uraisi.

Kama inavyoeleweka kuwa waandishi ni watu muhimu sana kwa wakati huu wapo ambao watatumiwa vibaya na wanasiasa na wapo watakaotumiwa vizuri lakini jambo la kuzingatia ni kudumisha amani na utulivu na kukumbuka kuwa baada ya uchaguzi kuna maisha, kwa maana kwamba wanahabari kamwe wasikubali kuwa chanzo cha matatizo ya nchi.

Uzoefu unaonesha wazi kwamba kila ifikapo kipindi cha uchaguzi baadhi ya vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla huwa ni sehemu ya chama cha kiasiasa hivyo basi husahau wajibu wao na ndio maana Tume ya Utangazaji Zanzibar mwaka 2015, ilitoa kitabu maalumu cha Muongozo wa Huduma za Utangazaji Wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Muongozo huo wa mwaka 2015, umebainisha vipengele kadhaa ambavyo ni wajibu wa mwandishi wa habari au taasisi ya habari kama vile gazeti, Televisheni v, radio au hata mitandao ya kijamii kuweza kuupitia, kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa mambo kwa mfano sehemu ya pili ya Muongozo huo umebainisha masuala ya midahalo ya kisiasa, matumizi ya simu katika vipindi, usawa katika utoaji wa habari na mengine kadha wa kadha.

Kwa kuwa muongozo huu wa Uchaguzi Mkuu umegawanywa katika sehemu tano ambapo katika Makala yetu hii tutaweza kugusia sehemu ya kwanza, ambapo imeeleza.

Muongozo huu utatumika na kuongoza watoaji wote wa huduma za utangazaji wanaofanya kazi Zanzibar, huku zikijumuisha uchaguzi mkuu, uchaguzi mdogo na uchaguzi wa marudio.

Katika kipengele hicho kwa hatua ya kwanza kimeeleza kitatumika kwa watoaji wa haduma za utangazaji waliopo Zanzibar. Iwe radio na Tv au Online Televisheni ama nyenginezo kwa kuwa vipo na kufanya shughuli zake Zanzibar, muungozo huu unawahusu kwa njia moja ama nyengine.

Labda unaweza ukajiuliza kwa nini Utangazaji? Ni kwa sababu ni njia nyepesi kuweza kusambaza habari kwa haraka kulinganisha na gazeti au Televisheni.

Radio ni chombe pekee cha habari kinacho wafikia wananchi kwa haraka zaidi, kuliko chombo chengine chochote cha habari.

Wanasiasa wengine hutumia radio kuwasilisha maudhui yao, yawe mazuri au mabaya kama daraja la kumvusha upande wa pili, bila husahau kwamba wa ni sehemu ya jamii na ndio mtaji wao wa kupata kura, hivyo basi ni vyema kuangalia athari ya vyombo vya habari kabla ya hatari kutokea.

Mifano ipo mingi karibu kila pembe ya dunia, lakini funzo zuri lipo kwa nchini wanachama wa Afrika ya mashariki kama vile Kenya, Rwanda, Burudi, Sudan, na hata Ethiopia, vyombo vya habari ndio vilichangia katika kuchochea vurugu kwa ajili ya kuwaridhisha baadhi ya wanasiasa waisiotakia mema nchi zao.

Ingawaje muuongozo huu unatumika zaidi Zanzibar tu, hivyo ni vyema kuwafahamisha wanahabari mipaka na wajibu wa kazi zao za kila siku.

Aidha waandishi wa habari na vyombo vya habari, ni jukumu lao kuupitia muongozo uliotolewa na Tume ya Utangazaji Zanzibar (2015), kwa sababu unatumika katika nafasi zote za wagombea kama vile Urais, Uwawakilishi, Ugunge na Udiwani.

Katika kipindi hiki cha msimu wa uchaguzi wapo baadhi ya waandishi au vyombo vya habari nchini, hutumika kama leso, leso ni miongoni mwa kitu muhimu, katika maisha ya watu wa mwambao wa Afrika Mashariki, ijapokuwa makala hiyo sio inayohusu Leso.

Neno Leso linaweza likawa na maana pana sana, kulingana na matumizi ya jamii husika.

Kwa mfano unapokutana na wenyeji wa Mombasa, Lamu au Pate nchini Kenya, neno Leso lina maana ya Khanga lakini katika jamii ya Tanzania Leso si khanga na upo uwezekano wa kuna na matumizi tofauti na khanga.

Hivyo, uchaguzi mkuu wa Oktoba baadhi ya wanasiasa, wanahabari na vyombo vyao ni msimu mzuri wa mavuno kwa kupitia migongo ya wanasiasa ambao wana uchu wa madaraka.

Lakini pia ni wakati mwafaka kwa baadhi ya waandishi kutumia kalamu zao kwa kuwapotosha, kuwatia khofu au kuwatisha wasomaji, watazamaji wa televisheni au wasikilizaji wa radio, ili mradi watimize yale wanayotaka kwa muda mchache, na ndipo ninapowasisitiza kuupitia muongozo uliotolewa na Tume ya Utangazaji Zanzibar kwani kuna mambo mengi ya kujifunza pamoja na kuyafanyia kazi.

Aidha ndani ya muongozo huu kuna ufafanuzi wa mambo mbali mbali kama vile:~ Huduma ya habari  ndani ya muongozo umeeleza kwamba ni huduma inayotolewa wa sauti, data, maandishi au picha ama zikiwa za mnato au zinazojongea isipokuwa pale ambapo zinafanayika kwa mawasiliano binafasi.

Mbali na hilo ufafanuzi mwengine ni kuhusiana na Matangazo ya kisiasa ambapo muongozo umebainisha kwamba ni matangazo yaliyolipiwa na yanayokusudia kuendeleza maslahi ya chama chohote cha kisiasa.

Kwa mantiki hiyo, basi waandishi wanatakiwa wawe makini katika kazi zao badala ya kuwa wasaka tonge, kwani kuna maisha baada ya uchaguzi na ni muhimu kuangalia maslahi ya taifa lako, jamii yako na haya watu wako.

Wapo wanaoheshimu kila mara hunukuu kwa kusema “kalamu ya mwandishi ni hatari kuliko bomu la atomic”, lakini pia baadhi yao hudiriki kusema “Endepo kalamu ya mwandishi wa habari itatumika vyema itasaidia katika ujenzi wa taifa na kinyume chake ni kuliangamiza taifa” na hili halitaki tochi kwani mifano ipo mingi hata katika baadhi ya nchi wanachama  wa jumuia ya Afrika ya Mashariki.

Inahuzunisha kwa baadhi ya wanasiasa, licha ya kwamba baadhi yao, wameupitia muungozo huo wa Tume ya Utangazaji Zanzibar 2015, lakini baadhi yao huwa ndio chachu ya kuwagawa waandishi wa habari na wapiga kura wao kama njugu na kuwafanya kama leso mara baada ya kufikia kileleni.

Wakati msaka tonge anapoitwa Muheshimiwa, kwako mwandishi  wa habari ni adui mkubwa na hakumbuki tena ihsani uliyomfanyia, kwa muda wote wa kutafuta kula badala ya kura.

Ifike wakati mwandishi wa habari afahamu wajibu wake katika jamii, kuliko kukurupuka na mbio za sakafuni, ambapo mwishio huishia ukingoni.

Kuacha kuupitia muongozo na kujuwa kilichoandikwa ndani ya muongozo huo ni khatari kwa chambo cha habari na hasa katika kipindi ambapo vyomba vya habari humea kama uyoga kila uchao.

Kwa vile huu ni msimu kwa baadhi ya wanahabari, naomba niwatanabahishe kuwa “mwendatenzi na omo, hurejea ngamani”, kukimbia kwao kwenye chumba cha habari, kwa kuwa tu ati yupo na mkuu fulani, kimbilio lako la mwisho huenda ikawa ni majuto ya Mussa na Firauni.

Ni aibu na fedha kwa waaandishi wa habari kuwa watumwa wa elimu na taaluma zao na ndio maana hata kwenye biblia imesema “Musipowashinda waandishi na mafarisayo ufalme wa mungu hamutaupata”, lakini pia kwenye biblia hiyo hiyo Yesu (Nabii Issa A.S) amesema “Sikuja kutengua taurati bali kutimiza taurati, lakini tazama kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya taurati ya bwana kuwa ni uongo”.

Hayo ni maneno matakatifu kutoka kwenye biblia, lakini pia kwenye qur-an karimu Mwenyezimungu amesema hivi “Naapa kwa kalamu na yale wayandikayo (kwa kalamu hizo).

Kwa kutumia vitabu hivyo vitakatifu, si dhani kama kuna mtu yoyote mwenye akili na ufahamu ambaye atapingana juu ya ukweli huo.

Kwa kupitia baraza la habari Tanzania, mwaka 2010 iliwahi kuchapisha kitabu maalumu chenye Kanuni za maadili kwa wanahabri, ambapo imelezwa kuwa “Mwandhishi wa habari anawajibu wa kueleza katika taarifa yake, mlolongo wa matukio yote kwa usahihi, uhakika na uwazi kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari na sheria zilizopo, zinalinda haki na makundi maalumu”.

Lakini pia, mwandishi wa habari anawajibika kupambanua lipi baya na zuri,katika utendaji wa kazi zake za kila siku, maoni  au tarifa zake ni lazima zizingatia maadili, ukweli na usahihi wa habari yake kabla ya kuitoa au kuichapisha, hatuoshi tu kuangalia hayo, lakini pia apime athari na faida kwa jamii yake.

Si hivyo tu, lakini pia, kuna baadhi ya waandishi wa habari nchini, wamekosa umaminifu katika kazi zao, na hasa ukiangalia kisingizo chao kikubwa kipato kitogo hakiendani na taaluma na kazi wanazofinya, na kama hilo lina ukweli kwa nini hutafuti kitu kingene chenye tija na ujira mzuri kuliko hii fani ya habari?

Kama hilo ni jambo la kupelekea mwandishi wa habari kuingia kwenye majaribu, kwa nini asishawishi kuongezewa mshahara kama ambavyo amekuwa akipigia debe taasisi nyengine?

Lakini ni jambo la ajabu sana kwa waandishi wa habari nchini ambao wengi wao hushia kwenye mikutano, semina, makongamano pamoja na mialiko ya kwenda kula na kunywa, kitu ambacho kinapeleka hata kusahau wajibu na haki zao za msingi kama waandishi wa habari na baadae kuwa leso kwa wala habari.

Katika karne ya 19, magazeti na majarida mengi ya ulaya yalijikita kwenye kampeni juu ya masuala ya kijami na kisiasa, ikiwa ni mabadiliko ambayo kwao waliona ni katika kuwavutia wasoji wao.

William Randolph Hearst na Joseph Pulitzer kwa uapande wao walijikita mara nyingi katika kuandika habari za kushtua jamii ambazo zaidi zilikuwa kwenye habari za uchunguzi, ambapo mara kadha walikuwa wakizungumzia juu ya uovu ulikuwa ukifanyika katika jamii zao.

Ni kinyume na hapa kwetu anaweza akasifiwa mtu hata kama hana sifa ilimradi tu, awepo kwenye chombo cha habari.

Kwa kuwa uandishi wa habari ni taalumu na fani maalumu kama zilivyo fani nyengine, kama vile sheria na udaktari, lakini ni jambo la kushangaza waliomo kwenye fani hii ya habari wengi wao hajuwi kitu kinachoitwa maadili, heshima wala utu wa mtu, kwao mshiko ndio kitu cha kwanza.

Inasikitisha kuona Tanzania kuna taasisi nyingi za kihabari,lakini hakuna moja ambayo wanachama wake wamefikia malengo, labda majungu, fitna na uhasama ndio ambao huongoza taasisi hizo.

Licha ya kwamba waandishi wa habari wapo mstari wa mbele kuwatetea wanasiasa, walimu, madaktari, lakini ni kichekisho kwamba wao wenyewe wameshindwa kujikomboa, licha ya kwamba kwa mataifa mengi uandishi ni muhimili wa nne katika mataifa hayo.

Taasisi kama MCT, UTPC, MISA-TAN, TAMWA, PRESS CLUB, na jumuiya ngengine za kihabari nchini zimekuwa mstari wa mbele katika kumtetea mwandishi wa habari, ikiwa ni pamoja na kuchapisha vijitabu kuhusiana na masuala ya maadili ya waandishi wa habari pamoja na vyombo vyao lakini wapi.

Bado wanahabari wamebakia kuwa ni leso kwa wanaojuwa kuwatumia, ni lazima  tufahamu kwamba kuna tofauti kubwa kati ya mwandishi na mwandishi wa habari, kwa kila mtu ni mandishi hata mwanasheri na daktari ni waandishi, lakini si waandishi wa habari, hii ni fani na yenye thamni kwa mwenye kujithamini.

Nasikitika kusema kwamba, waandishi wengi wa habari wa Tanzania hawajuwi umuhimu wao kama ambavyo msanii Mrisho Mpoto alivyo sema kwenye nyimbo yake ya “UHURU WANGU UKO WAPI” hii ni nyimbo maalumu kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini.

Lau kama mwandishi wa habari angejuwa thamani yake kwa taifa na jamii kwa ujumla, asingekubali kuwa leso, nasema leso ni kwa sababu ni mara ngapi tumesikia kuna waandishi wameachwa kwenye misafara, kudhalishwa hata kupigwa.

Jibu unaweza sema hapana, lakini ujiulize ni mara ngapi waandishi wameandika sakata la ESCROW, fedha kharamu, kashifa, wizi na ubadhirifu wa mali za ummah, cha ajabu waandishi wa habari wakatoa na jina ati “UFISADI”. Waandishi wa habari wanaogopa kusema Fulani mwizi na ni kweli mwizi na sikuchota vijisenti.

Kwa kuwa kipindi ni cha mavuno, kitu cha kuzingatia ni kujiuliza unavuna nini?. Maadili katika kuandiaka au kuandaa habari za uchaguzi ni kitu cha msingi sana.

Ni lazima tuzingatie kwamba, mtoa wa huduma za utangazaji ni mtu aliyepewa leseni, anayetoa huduma ya utangazaji chini ya na kulingana  na vifungu vya sheria na masharti ya leseni  iliyotolewa na Tume.

Kwa mnasaba huu basi unaposoma sehemu ya kwanza ambayo imesishia kwenye uafafanuzi utaona sehemu kubwa imegusia Utangazaji ama Televisheni au Radio, hii ni kuonesha vyombo hivi ndio hutoa taarifa kwa haraka zaidi kuliko vyengine.

Kitu cha kuzingatia kwa sasa kila mtu awe na hadhari kuhusiana na kutangaza suala zima la uchaguzi nchini kwa ajili ya kudumisha amani na utulivu nchini huku tukizingatia ile kauli nzuri isemayo baada ya uchaguzi kuna maisha.

CAP

MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC ) Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Hamid Mahmoud, akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya Zanzibar, kuhusiana na utoaji wa taarifa ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwa Urais, Uwakilishi na Udiwani, unaotarajiwa kufanyika mwaka huu 2020. (Picha na Abdalla Omar)