NA MWAJUMA JUMA
TUZO ni chachu inayompa nguvu mtu yoyote ambaye atatunikiwa kutokana na jambo zuri alilofanya, kama ni sehemu ya kumpa moyo ili kuendelea na mazuri yake.
Hivyo basi ni wazi kuwa kitendo cha kutoa tuzo ni tukio muhimu ambalo linapaswa kufanya na taasisi yoyote, kwa watu wake ili kuwapa moyo zaidi wa utendaji.

Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa wasanii ambao ni sehemu muhimu ya jamii, inahitaji kupewa tuzo, ambapo tuzo hizo zitakuwa na zawadi nono, ili kuleta hamasa kwa wasanii wengine kufanya kazi zao ziwe katika hali nzuri.

Msanii akiona mwenzake amepata tuzo itamfanya kujenga bidii ili na yeye kupata zaidi ya aliyopata mwezake, hali ambayo itasaidia msanii kupambana zaidi kushinda.
Siku za hivi karibuni kulifanyika tukio la utoaji wa tuzo ya Mfuko wa Emerson,

ambapo tuzo hiyo licha ya kuwepo kwa filamu nyingi lakini hakupatikana mshindi.
Mshindi katika tuzo hiyo iliyoshirikisha filamu 21 za Kizanzibari, hakupatikana kwa kile killichoelezwa kuwa filamu zilikosa viwango.

Kama hiyo kweli ni vyema basi vyombo vinavyosimamia sanaa kuangalia suala hili kwa umakini mkubwa na kutafakari kwa undani.

Emerson katika tuzo hiyo walitaja karibu vigezo 10 ambavyo walitoa ili kushindaniwa.
Vigezo vyengine ni jinsi filamu ilivyosanifiwa pamoja na mtiririko wa vitendo, lugha iliyotumika kwenye filamu, mchango wa filamu kwa utamaduni wa Zanzibar na walivyoshiriki au walivyoshirikishwa wazanzibari.

Binafsi nalitizama suala hilo kwa umakini mkubwa na kubaini kuwa, kushindwa kupata tuzo hiyo ni fedheha na wasanii wanapaswa kukaa na kutafakari hili.

Hivyo basi kazi ya Baraza la Sanaa kulifuatilia hilo na kuweza kuwakusanya wasanii, ili kuona wanafanya vipi kazi zao hadi kushindwa kufikia vigezo.

Baraza ndio wasimamizi wa kazi za wasanii, hivyo wanapaswa kutoa elimu ya kutosha kwa watengenezaji wa filamu ili kuzaa filamu zenye ubora.
Hapa Serikali kupitia Baraza la Sanaa na Filamu linapaswa kutoa elimu kwa wasanii, namna ya utengenezaji wa filamu na kufuatilia kwa kina vigezo ambayo vinatakiwa kutumika kwa waandaaji wa filamu hizo.

Zanzibar Wasanii wapo wengi lakini wengi wao elimu yao ni ndogo na wanafanya kazi kwa mazowea, jambo ambalo kwa sasa limepitwa na wakati.

Hivyo basi ni wazi kuwa wanahitaji usimamizi wa hali ya juu ikiwa pamoja na kuwapa elimu, katika kusimamimia taasisi kama hizo na kuziendesha.
Likishindwa kufanyika hilo maana yake ni kuwa watajikuta kuna vyama vingi lakini kila siku vitaendelea kuilalamikia wizara,idara au baraza.

Tunahitaji mpango mkakati kama nchi ili kuifanya sanaa kuwa ajira ya kweli , inufaishe msanii na kuchangia pato la nchi, vinginevyo miaka nenda miaka rudi hakutakuwa na mfanikio yoyote.