GITEGA,BURUNDI

MAMIA ya wakimbizi raia wa Burundi walioko nchini Rwanda wameanza kurejea nchini kwao, miaka mitano baada ya kukimbia mapigano na ghasia za kisiasa.

Wakimbizi karibu mia tano wa Burundi walirejea nchini kwao Alkhamisi,likiwa ni kundi la kwanza la wakimbizi Warundi kurejea nchini,tokea nchi hiyo ishuhudie machafuko ya kisiasa yaliyosababishwa na hatua ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza, kugombea muhula wa tatu kinyume na katiba ya nchi.

Warundi hao walinukuliwa na vyombo vya habari wakisema kuwa, waliamua kurejea nyumbani wakiwa na imani ya kutengeneza mustakabali wao na wa taifa lao, kwa kuwa nchi hiyo hivi sasa ina kiongozi mpya.

Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi alichukua hatamu za uongozi mwezi Juni mwaka huu, kurithi mikoba ya Pierre Nkurunziza.

Kabla ya kuwasili basi la kuwasafirisha kwenda Burundi wakitokea Rwanda, wakimbizi hao walifanyiwa vipimo vya ugojwa wa Covid-19.

Siku chache nyuma, watu 15 waliuawa baada ya watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha kushambulia wakaazi wa eneo moja huko kusini mwa Burundi.

Ofisa mmoja wa Serikali ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema shambulizi hilo lilifanywa na waasi wanaopinga mpango wa Serikali wa kuanza kuwarejesha nchini wakimbizi raia wa nchi hiyo walioko Rwanda. 

Rwanda ni mwenyeji wa makumi ya maelfu ya wakimbizi kutoka nchi jirani ya Burundi, waliokimbia vita na mapigano nchini kwao tokea mwaka 2015.