HUKU uchaguzi mkuu wa Marekani ukijongea, ambapo mchuano utakuwa mkali baina ya rais wa sasa anayetetea nafasi yake Donald Trump na makamu wa rais wa zamani Joe Biden.

Uchaguzi huo umekuwa ukivuta hisia kubwa sio tu kwa wananchi wa Marekani bali hata mataifa ya nje, ambapo yapo yanayona bora nchi hiyo ipate kiongozi mwengine na yapo mataifa yanayoona bora Trump aendelee.

Katika mataifa ambayo yanatajwa kuwa na ushawishi mkubwa kwenye uchaguzi wa Marekani ni pamoja na China, Urusi na Iran, huku idara za ujasusi nchini Marekani zikitahadharisha ushawishi wa mataifa hayo.

Katika uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2016, zipo taarifa kwamba Urusi ilihusika kwa kiasi kikubwa kuingilia uchaguzi huo kiasi cha kumuwezesha Donlad Trump kushinda nafasi hiyo.

Wasiwasi wa uingiliaji kati kwenye uchaguzi mkuu wa Marekani unazidi hasa kufuatia juhudi kubwa zilizofanywa na Urusi kuingilia uchaguzi wa mwaka 2016 kwa niaba ya Trump kupitia udukuzi wa mfumo wa barua-pepe wa chama cha Democratic na kampeni ya siri ya mitandao ya kijamii iliyolenga kusababisha mtafaruku miongoni mwa wapigakura wa Marekani.

Hata hivyo, Trump mara zote anapinga madai kwamba Kremlin ilimpendelea mwaka 2016, lakini tathmini ya mashirika ya ujasusi iliyotolewa inaonesha kuwa watu wenye mafungamano na Kremlin ambao hawakutajwa majina, wanafanya kazi kuimarisha kampeni za Trump kwenye mitandao ya kijamii na televisheni nchini Urusi.

Kwenye uchaguzi wa mwaka huu taarifa za idara za ujasusi nchini Marekani zimebainisha kuwa yapo mataifa yanajaribu kutumia ushawishi kuyumbisha zoezi la uchaguzi huo.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa idara hiyo ilisema nchi za kigeni zinatumia njia za ushawishi na kwamba China ingependa kuona Donald Trump hachaguliwi kwneye uchaguzi huo utakofanyika mwezi Novemba mwaka huu.

Idara hiyo ilifafanua kuwa kwa upande wa Urusi ingependa kumuona Trump anaongoza kwa muhula mwengine tena na kwamba isingependa kabisa kumuona Joe Biden anaongoza taifa hilo.

Wakuu wa idara za ujasusi wanasema Urusi ilitaka kusaidia kuongezea nguvu kampeni za Trump, ikiwemo kueneza habari za uongo mtandaoni dhidi ya Joe Biden.

William Evanina, mkuu wa kituo cha kitaifa cha usalama na kupambana na ujasusi (NCSC), alitoa taarifa ya ripoti inayoelezea ushawishi wa mataifa hayo katika uchaguzi mkuu wa Marekani.

“Nchi za kigeni zinajaribu kupendelea matakwa ya wapiga kura, kubadilisha sera za Marekani, kuongeza mizozo nchini na kudhoofisha imani ya watu wa Marekani katika mchakato wetu wa demokrasia”, alisema Evanina.

Hata hivyo, William alisema kuwa itakuwa vigumu kwa mataifa hayo aliyoyaita kuwa ni maadui kufanikiwa kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka huu hasa ikizingatiwa kuwa Marekani imejipanga kukabiliana na hali hiyo.

Taarifa hiyo ya Evanina inaaminika kuwa tangazo la wazi kabisaa kutoka kwa jumuiya ya ujasusi ya Marekani, kuhusisha juhudi za ikulu ya Kremlin kumsaidia Trump achaguliwe tena.

“Nchi nyingi zina upendeleo kuhusu nani ashinde uchaguzi, alisema, na kuongeza kuwa macho ya Marekani yatakuwa kuziangalia kwa karibu nchi tatu zikiwemo China, Urusi na Iran:

China inapenda kuona Trump akikikosa kiti hicho taarifa hiyo imeeleza na kuongeza kuwa China imekuwa ikiongeza jitihada za ushawishi kabla ya kura.

Urusi inatafuta kupaka matope nafasi anayoiwania Biden huku washirika wenye uhusiano na Urusi piia wanatafuta kumpiga jeki Trump kwenye mitandao ya kijamii na televisheni.

Moscow isingependa kumuona Biden anashinda kwa sababu inaamini kiongozi huyo anaweza kuendeleza sera za Barack Obama za kuishindikiza na kuiminya Urusi.

Putin na Trump

Wakati wa utawala wa Obama ambapo Biden alikuwa makamu wa rais, aliisaidia sana nchi ya Ukraine ambayo imekuwa na uhasama wa muda mrefu na Urusi jambo ambalo Urusi inaona huenda likajirejea.

Iran inajaribu kudhoofisha taasisi za chama cha Democratic Marekani , Trump na kuigawanya nchi kwa kusambaza taarifa za uongo na maudhui kuipinga Marekani mtandaoni.

Jitihada zao zinasukumwa na imani kuwa muhula wa pili wa rais utasababisha muendelezo wa shinikizo la Marekani juu ya jitihada za kuchochea mabadiliko ya utawala nchini Iran.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika hivi karibuni, Trump alisema Urusi inaweza kuingilia uchaguzi wa mwaka huu, lakini ilitupilia mbali wazo kwamba nchi hiyo inaweza kuwa inajaribu kumsaidia kushinda muhula wa pili.

“Ninadhani mtu wa mwisho Urusi inataka kuona ikishinda ni Donald Trump,” alisema, hakuna mtu ambaye amekuwa mkali kwa Urusi kuliko mimi”, aliongeza.

Aliongeza kwa kusema “angalia tulivyofanya na jeshi letu, angalia tulivyofanya katika kuweka wazi suala la bomba ambapo mabilioni yanakwenda Urusi. Angalia mambo yote tuliyoyafanya na NATO”, alisema Trump kuonesha uthibitisho jinsi alivyoibana Urusi wakati wa utawala wake wa miaka minne.

China itapenda ikiwa itashuhudia Trump akipoteza kiti hicho, ambapo Trump mwenye alisema kama Biden atashinda wachina wataimiliki Marekani.

Kutolewa kwa taarifa hiyo kunakuja baada ya wanachama wa chama cha Democratic kueleza wasiwasi wao kuhusu majaribio ya mataifa ya nje kushawishi kura.