BEIRUT,LEBANON

MAWAZIRI wawili wa serikali ya Lebanon wamejiuzulu kufuatia mripuko mbaya ambao ulichochea ghadhabu ya umma dhidi ya utawala wa nchi hiyo, huku waandamanaji wakikabiliana na polisi katika mji mkuu wa Beirut kwa siku ya pili.

Waziri wa habari Manal Abdel Samad na Waziri wa Mazingira Damianos Kattar,wote walitangaza kujiuzulu, ikiwa ni pigo jengine kwa Serikali ya Waziri Mkuu Hassan Diab.

Wabunge kadhaa pia wanaripotiwa kuachia ngazi na vyombo vya habari vya ndani vinasema Diab anafikiria kutangaza kujiuzulu kwa Serikali yote, siku moja baada ya waandamanaji kuyadhibiti kwa muda majengo ya Wizara.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alikuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa ulioahidi kiasi cha uro milioni 250 kwa ajili ya kuisaidia Lebanon ambako kiasi ya raia 300,000 walikosa makaazi kutokana na mkasa huo.