BEIRUT,LEBANON
TAIFA la Lebanon linaomboleza baada ya mripuko mkubwa katika mji mkuu wa Beirut uliopelekea zaidi ya watu 100 kuuawa na wengine zaidi ya 4000 kujeruhiwa.
Mripuko huo ulitokea katika ghala nambari 12 la Bandari ya Beirut na kwamba sababu ya moto ni mada za miripuko ambazo zilikuwa zimehifadhiwa hapo.
Mripuko huo ulikuwa mkubwa kiasi cha kusikika kilomita nyingi kutoka eneo la tukio.
Taarifa zaidi kutoka mji mkuu wa Lebanon Beirut zinasema kuwa, mripuko huo ulisababisha hasara kubwa kwa nyumba za makaazi na pia katika idara binafsi na za Serikali hasa majengo yaliyokuwa karibu na tukio hilo.
Mataifa mbalimbali yalitoa salamu za rambirambi na mkono wa pole kwa Serikali na wananchi wa Lebanon na kutangaza kuwa pamoja na taifa hilo katika kipindi hiki kigumu hasa kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa pamoja walituma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha kwenye matukio hayo huku akiwatakia kupona haraka majeruhi.

Iran kupitia Waziri wake wa Mashauri ya Kigeni Dakta Muhammad Javad Zarif ilituma salamu za mkono wa pole na za kuliwaza kwa taifa la Lebanon.
Aidha Syria, Iraq, na Yemen ni miongoni mwa mataifa yaliyotuma salamu za mkono wa pole kwa Serikali na wananchi wa Lebanon.
Rais Michel Aoun aliitisha kikao cha dharura jana huku akitangaza hali ya hatari ya wiki mbili nchini humo.