LISBON, Ureno
KLABU ya Ligi Kuu ya Ujerumani ya RB Leipzig imetinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuifunga Atletico Madrid magoli 2 – 1, katika mashindano yanayoendelea jijini Lisbon, Ureno.

Kikosi hicho kinachonolewa na kocha Julian Nagelsmann kilipata ushindi huo baada ya kuonyesha mchezo mzuri dhidi ya miamba hiyo ya Hispania, licha ya kutokuwa na mshambuliaji wao nyota, Timo Werner aliyehamia Chelsea.

Leipzig sasa itakutana na Paris Saint-Germain Jumanne ijayo. PSG inayofundishwa na Mjerumani Thomas Tuchel iliichapa Atalanta Bergamo magoli 2 – 1 katika dakika ya mwisho siku ya Jumatano.

Jana kulitarajiwa kufanyika pambano kali kati ya mabingwa wa ‘Bundesliga’ Bayern Munich dhidi ya miamba ya Hispania ya FC Barcelona. (AFP).