NA MWANDISHI WETU
KATIKA mwaka 1960, serikali ya Urusi ilianzisha kituo kidogo cha utafiti katika eneo la Novolazarevskaya lenye baridi kali katika mwambao wa bahari Antatiki kaskazini mwa Ulaya.
Kikundi hicho cha watafiti kilikuwa na wanasayansi 13 ambao Leonid Rogozov alikuwa ni daktari pekee katika kundi hilo.
Leonid Rogozov
Leonid Ivanovich Rogozov alizaliwa mwaka 1934 katika kijiji cha Chita Oblast huko Siberia ya mashariki kijiji ambacho kiko katika mpaka wa Urusi na China na Mongolia.
Baba yake mzazi aliuawa katika vita vya pili vya dunia mwaka 1943. Alimaliza masomo ya sekondari katika mwaka 1953 huko Minusinsk na kisha kuchaguliwa kujiunga na taasisi ya tiba ya “Saint Petersburg State Pediatric Medical Academy” na kuhitimu masomo yake ya utabibu hapo mwaka 1959.
Akiwa na umri wa miaka 26 hapo Septemba, 1960 ndipo alipotakiwa kukatisha masomo yake ya shahada ya pili ya tiba kwa muda na kuungana na kundi la watafiti waliopelekwa na serikali ya Urusi huko Novolazarevskaya akiwa ni daktari pekee.
Asubuhi ya Aprili 29, 1961 daktari huyo alianza kupoteza nguvu mwilini na kuhisi maumivu makali hasa upande wa kulia wa tumbo lake. Kutokana na uzoefu wake wa udaktari alijua kuwa alikuwa na tatizo la kidole tumbo (appendix).
Hali ya daktari Leonid Rogozov ilizidi kuwa mbaya siku ya pili yake ambapo kibaya zaidi ni kwamba kituo hicho kilikuwa mbali mno na maeneo mengine yenye huduma za afya.
Si hayo tu, kutokana na hali mbaya ya hewa ya theluji nzito na vimbunga vya theluji vilivyopiga mara kwa mara eneo la Novolazarevskaya halikuweza kufikika kwa ndege.
Kituo chengine cha utafiti kutoka eneo hilo ni kile cha Mirny ambacho kilikuwa umbali wa maili 1,000. Hata safari ya meli kutoka Urusi hadi eneo la kituo hicho katika bahari ya Antatiki ilichukua siku 36. Kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya, daktari huyo alifanya tukio lisilo la kawaida la kujifanyia upasuaji mwenyewe kuondoa tatizo hilo.
Daktari Leonid Rogozov, alianza kujifanyia upasuaji saa nane mchana siku ya tarehe 1 Mei, 1961 akisaidiwa na dereva na mtabiri wa hali ya hewa.
Dereva alikuwa na kazi ya kumsogezea daktari huyo vifaa vya upasuaji na mtabiri wa hali ya hewa alimuwekea kioo na taa kuweza kuona sehemu za ndani za tumbo ambazo alikuwa akizikata kwa kutumia vifaa vya upasuaji.
Kwa kutumia uzoefu wake wa upasuaji, Daktari Rogozov kabla ya kuanza upasuaji huo, aliwafahamisha wasaidizi wake jinsi ya kumchoma sindano iwapo ingehitajika na nini wafanye iwapo atapoteza fahamu.
Alijilaza kujipasua upande wa kushoto na kutumia dawa aina ya ‘novocain’ kupunguza maumivu. Rogozov alijipasua tumbo lake tundu yenye upana wa sentimita 12.
Ingawa aliekewa taa kuongeza mwangaza, lakini alilazimika kutumia tochi kwa vile kutokana na jinsi alivyokuwa amelala asingeweza kuona sehemu ya ndani ya tumbo lake kwa kutumia taa ya kawaida.
Wakati akiendelea na upasuaji huo, daktari huyo kwa bahati mbaya alikata sehemu ya ndani ya ngozi nyembamba ya tumboni ‘peritoneum’ na hivyo akalazimika kushona ngozi hiyo kabla ya kuendelea na upasuaji huo.
Ukweli ni kwamba kidole tumbo kilichokuwa kikimsumbua kilikuwa na uvimbe mweusi sehemu ya chini na kama asingelifanya upasuaji huo basi kidole tumbo hicho kingepasuka katika siku chache za usoni na kingesababisha kifo cha daktari huyo.
Licha kwamba alitumia dawa kadhaa za kutuliza maumivu, lakini alilazimika kupumzika kwa muda wa dakika 30 na kisha kuendelea na upasuaji huo ambao ulimalizika saa 10 jioni.
Baada ya upasuaji huo kumalizika salama, daktari huyo aliwafahamisha wasaidizi wake namna ya kusafisha vifaa vya upasuaji na chumba alichofanyia upasuaji wake na baada ya kuridhika kuwa vifaa hivyo na chumba viko katika kiwango kinachohitajika kwa kanuni za matibabu ndipo alipokula vidonge vya kupunguza machungu na kupata usingizi.
Rogozov alianza kurejea katika hali ya kawaida kiafya ambapo baada ya siku tano, aliweza kuinuka na kufanya mazoezi na nyuzi alizoshonea tumbo lake alizitoa baada ya wiki moja.
Kitendo cha daktari huyo kujifanyia upasuaji wa kidole tumbo, kilileta hisia mchanganyiko miongoni mwa wananchi wa Urusi kwa wakati huo ambapo kutokana na tukio hilo serikali ya taifa hilo iliweka madakari zaidi ya mmoja katika vituo vyote ya mbali vya utafiti na shughuli nyengine.
Mwaka huo huo wa 1961, Daktari Rogozov alitunukiwa nishani ya “Order of the Red Banner of the Labour”.
Nishani hiyo hutolewa nchini Urusi kwa mfanyakazi, mvumbuzi au taasisi yeyote ya taifa hilo kuthamini mchango uliotolewa na mtu au taasisi fulani katika uzalishaji, sayansi, uvumbuzi, sanaa, ubunifu, elimu au mchango wowote ule unaosaidia jamii.
Katika mwezi wa Oktoba, 1962, Daktari Rogozov alirejea katika mji wa Leningrad na kuanza kufanya utafiti wa shahada ya pili ya utabibu. Katika mwezi wa Septemba 1966 alichapisha andiko lake la utafiti liitwalo “Resection of the esophagus for treating esophageal cancer”.
Baadae alifanyakazi katika hospitali kadhaa katika mji wa Leningrad ambapo kati ya mwaka 1986 hadi 2000 alikuwa ni Mkuu wa upasuaji katika Taasisi ya Utafiti wa Kifua Kikuu ya mji wa Saint Petersburg.
Daktari Rogozov alifariki dunia kutokana na kensa ya Ini mwaka 2000 huko Saint Petersburg.