TRIPOLI, LIBYA

SERIKALI  ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imetangaza kuweka kafyu katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli kufuatia kushamiri  kwa maandamano ya wananchi.

Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya ilitoa taarifa na kueleza kuwa, zuio hilo la kutotoka nje linaanza kutekelezwa kuanzia jana saa tatu asubuhi hadi saa 12 jioni.

Tangazo la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya linaeleza kuwa, kwa siku za Ijumaa na Jumamosi, kafyu hiyo itatekelezwa kwa muda wa masaa 24. 

Serikali ya Libya ilichukua uamuzi huo baada ya kundi la waandamanaji kuvamia makaazi ya Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya.

Tripoli mji mkuu wa Libya uligubikwa na maandamano dhidi ya Serikali tangu Jumapili iliyopita. Wafanya maandamano wanataka kupinduliwa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya.

Wafanya maandamano huko Libya wanasema kuwa Serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al Sarraj ni chanzo cha kukosekana mahitaji muhimu nchini humo kama maji, umeme na wafanyakazi kushindwa kulipwa mishahara na mafao yao.

Wafanya maandamano huko Libya wanataka katiba ya nchi  hiyo ifanyiwe marekebisho, kufanyike uchaguzi huru na wa haki na kuendeshwe mapambano dhidi ya ufisadi.