NA MWAJUMA JUMA

LIGI daraja la Kwanza kanda ya Unguja inatarajiwa kuendelea kesho Alkhamis ambapo jumla ya mechi nne zitachezwa katika viwanja vya Mao Zedong.

Ligi hiyo ilisimama baada ya Serikali kupiga marufuku mikusanyiko kutokana na maradhi ya virusi vya corona, ratiba inaonesha kuwa mechi mbili zitachezwa wakati wa saa 8:00 mchana na mbili saa 10:00 za jioni katika viwanja vyote viwili.

Wakati wa saa 8:00 mchana kwenye uwanja wa Mao Zedong A Miembeni itacheza na Mwememakumbi City,uwanja wa Mao Zedong B Black Sailor itashuka kupambana na Kikwajuni.

Aidha wakati wa saa 10:00 za alaasiri Mao Zedong A Idumu
itakwaruzana na Bweleo na Mao Zedong B Mundu kutoka Nungwi itakuwa uso kwa uso na Dula Boys ya Jambiani.

Ratiba hiyo pia inaonesha kuwa siku ya Ijumaa kutakuwa na michezo miwili ambayo yote itachezwa wakati wa saa 10;00 za alaasiri ambapo Mao Zedong A Taifa ya Jang’ombe itacheza na Mchangani na Mao Zedong B Uhamiaji itapambana na Ngome.

Wakati ligi hiyo inasimama Taifa ya Jang’ombe ndio inayoongoza kwa kuwa na pointi 34 akifatiwa na Black Sailor ambao wana pointi sawa lakini Taifa yupo mbele kwa mchezo mmoja.

Nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi hiyo inashikiliwa na Uhamiaji yenye pointi 30, wakati Idumu inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 26 na nafasi ya tano inakamatwa na Mchangani wenye pointi 27.

Timu ambazo zipo hatarini kushuka katika ligi hiyo mpaka sasa ni Mundu wenye pointi 18 nafasi ya 10, Bweleo yenye pointi 18 nafasi ya 11, Miembeni wapo nafasi ya 12 pointi 14 na Kikwajuni wanashika mkia akiwa na pointi 14 pia.