LISBON, Ureno

MOUSSA Dembele aliingia uwanjani kipindi cha pili na kufunga mabao mawili ya dakika za mwisho, wakati Lyon ikiishangaza Manchester City kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

City ilionekana kuwa bora zaidi ya wapinzani kwa kumiliki mpira muda mrefu, lakini walishindwa kutumia vyema nafasi nyingi walizozipa kufunga mabao.

Lyon ilianza kupata bao la mapema lililofungwa na Maxwel Cornet katika kipindi cha kwanza, ambalo lilidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Kipindi cha pili Kevin De Bruyne aliweza kuiswazishia City na kuufanya mchezo huo kuwa mzuri na kuendelea kushambuliana zaidi kila upande ukisaka bao la ushindi.

Mabao ya ushindi ya Lyon yalifungwa na Moussa Dembele kwenye dakika za 79 na 87.

Kinyume na matarajio yote, timu iliyomaliza katika nafasi ya saba katika msimu wa kandanda la Ufaransa, na ambayo ilikuwa imecheza mechi mbili pekee za ushindani tangu mapema Machi, sasa itacheza katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Jumatano dhidi ya Bayern Munich.

Hiyo bila shaka ni hatua kubwa kwa timu hiyo ya Rudi Garcia na lakini pia hakuna aliyetarajia kuwa wangewaondoa Juventus katika duru ya mwisho, achia mbali kuwaondoa City katika hatua ya robo fainali.

“Bado tuko mashindanoni, kumaanisha kuwa tuna timu nzuri,” Mshambuliaji wa zamani wa Celtic Dembele aliiambia televisheni ya Ufaransa ya RMC Sport. “Tunazungumzia mechi moja baada ya nyingine, hatutajisahau. Tutajaribu kuwa tayari kuvaana na Bayern.

Timu hiyo ya Guardiola ilikuwa imepewa onyo na Lyon, kwa kushindwa nyumbani na kisha kutoka sare ugenini dhidi ya klabu hiyo ya Ufaransa katika Ligi ya Mabingwa msimu uliopita. Lakini hiyo ilikuwa karibu miaka miwili iliyopita na Lyon imepoteza wachezaji kadhaa muhimu tangu wakati huo.

Matokeo haya, siku moja baada ya Bayern kuibomoa Barcelona 8 – 2, ni mshtuko mkubwa na pigo kubwa kwa malengo ya City chini ya Guardiola.

Subira yao ya kushinda Kombe la Ulaya itaendelea, hii ikiwa ni mara ya tatu mfululizo kuondolewa katika robo fainali.