ABUJA,NIGERIA

KITUO cha Kukinga na kudhibiti Magonjwa cha Afrika (Afrika CDC) kimesema hivi sasa nchi 32 za Afrika zimeripoti chini ya maambukizi 5,000 ya ugonjwa wa Covid-19, huku maambukizi mapya yakiongezeka kwa kasi katika nchi chache barani humo.

Kituo hicho cha Umoja wa Afrika kimesema nchi nane barani Afrika ziliripoti maambukizi mapya kati ya 5,000 hadi 10,000, na nchi nyengine 11 zilirikodi maambukizi kati ya 10,000 na 50,000.

Kwa mujibu wa takwimu hizo zilizotolewa na Afrika CDC, hadi kufikia sasa Afrika Kusini ndiyo nchi pekee iliyoripoti maambukizi zaidi ya 10,000 barani humo, na kufanya idadi ya maambukizi nchini humo kupindukia laki sita. Aidha idadi ya vifo vya corona nchini humo imefikia 13,059.

Watu zaidi ya milioni moja na 183,000 wameambukizwa virusi vya corona barani Afrika.Watu 27,652 wamefariki dunia kwa maradhi ya Covid-19 barani humo.

Zaidi ya watu milioni 23 na laki sasa wamepatwa na virusi vya corona na zaidi 813,000 wamefariki dunia kutokana na virusi hivyo kote duniani. 

Aidha wagonjwa zaidi ya milioni 15.3 wa corona wamepata afueni duniani kote.