NA MARYAM HASSAN

KUWEPO kwa malalamiko juu ya maamuzi yanayotolewa na mahakama ya ardhi kumesababisha baadhi ya wananchi kupaza sauti zao katika vyombo vya habari kuilalamikia mahakama hiyo.

Hali hiyo imejitokeza hivi karibuni kwa baadhi ya wananchi kutoa malalamiko yao katika chombo cha habari kwa kudai kuwa hawakuridhika na maamuzi yanayotolewa na mahakama hiyo.

Malalamiko hayo yamekuja juu ya shauri lililowasilishwa mahakamani hapo la Amour Duchi linalohusu mgogoro wa ardhi ambalo lilitolewa maamuzi hivi karibuni na kupelekea kuibuka kwa mzozo mkubwa.

Shauri hilo inaelezwa kuwa mlalamikaji huyo alishinda huku sababu kubwa iliyopelekea kupata ushindi huo ni kuwa wadaiwa wameshindwa kufika mahakamani kila tarehe inayopangwa kwa ajili ya kusikilizwa.

Aidha kwa upande wa Boniface Joseph ambae nae analalamikiwa kuvunja nyumba ya watu huko Welezo nae alisema alifanya hivyo kwa sababu ya maamuzi yaliyotolewa mahakamani hapo.

Akijibu hoja hizo Mwenyekiti wa mahakama ya Ardhi Vuga Khamis Rashid Khamis alisema maamuzi yote yaliyotolewa mahakamani hapo yametolewa kisheria.

Alisema mahakama ya adhi ni chombo mahasusi kilichoundwa chini ya sheria nambari 7 ya mwaka 1994, kikiwa na mamlaka ya kutatua migogoro mbali mbali inayohusiana na ardhi.

Alisema kitendo cha wananchi kufikisha malalamiko yao katika vyombo vya habari hakileti picha nzuri, kwa sababu tayari kimeundwa chombo mahsusi kwa ajili ya kusikiliza hoja hizo.

Alisema kulalamika katika vyombo vya habari si sahihi kwa sababu havina mamlaka ya kutengua maamuzi yaliyotolewa na mahakama, hivyo aliwataka wananchi kuacha kufanya hivyo na badala yake wafuate sheria.

Akizungumzia kuhusu suala la Boniface Joseph alisema zaidi ya vikao vitatu wameitwa wadaiwa mahakamani lakini wameshindwa kuhudhuria vikao hivyo kwa ajili ya kupata ufumbuzi.

Pia alifahamisha kuwa Juni 26 mwaka jana walipeleka tangazo la wito ZBC juu ya kuwaita wadaiwa hao lakini pia wameonekana kudharau.

Hivyo kupitia kifungu cha 38 sheria ya mahakama ya Ardhi ya mwaka 1994 wamelazimika kusikiliza shauri hilo upande mmoja (expart judgement) pasina kuwepo wadaiwa na kutoa maamuzi yanayofaa kisheria.