BANGKOK,THAILAND

ZAIDI ya watu elfu moja wameandamana jana kwenye mji mkuu wa Thailand, Bangkok, kushinikiza kujiuzulu kwa Serikali, mabadiliko ya katiba na kukomeshwa unyanyasaji unaofanywa dhidi ya wanaharakati wa upinzani.

Pamoja na kutoa wito wa kujiuzulu kwa Waziri mkuu Prayuth Chan-ocha aliyeshinda uchaguzi uliogombaniwa mwaka uliopita, waandamanaji pia wanataka kupunguzwa kwa nguvu za familia ya kifalme.

Waandamanaji walikusanyika mbele ya mnara wa demokrasia mjini Bangkok kwa maandamano makubwa kuwahi kuhushuhudiwa tangu Prayuth aliyewahi kuwa kiongozi wa jeshi alipochukua madaraka kwa mapinduzi mwaka 2014.

Waandamanaji walisema mkusanyiko wa jana utadhihirisha jinsi umma unavyounga mkono mageuzi katika taifa hilo la kusini mashariki ya bara la Asia.