MINSK,BELARUS

LICHA  ya ukandamizaji mkubwa wa polisi, maandamano ya kupinga mtokeo ya uchaguzi yameendelea kwa usiku wa tatu mfululizo nchini Belarus, hata baada ya mgombea mkuu wa upinzani kukimbilia nchini Lithuania.

Umoja wa Ulaya ulionya juu ya uwezekano wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo.

Mpinzani mkuu wa Rais Alexander Lukashenko katika uchaguzi huo, Sviatlana Tsikhanouskaya, ambaye alishiriki kinyang’anyiro hicho baada ya mume wake kufungwa jela, aliwaomba radhi waungaji wake mkono katika ujumbe wa vidio, na kusema lilikuwa chaguo lake kuondoka nchini humo.

Katika ujumbe mwengine wa vidio uliotolewa, aliwahimiza wafuasi wake kuheshimu sheria na kuepuka makabiliano na polisi, licha ya hapo awali kupinga matokeo yaliompa ushindi mkubwa rais Lukashenko.

Maelfu ya wafuasi wa upinzani wanaopinga matokeo ya uchaguzi huo, walikabiliana na polisi katika mji mkuu, Minsk pamoja na miji mingine kadhaa ya Belarus.