NA SHAIB KIFAYA

VIFAA tiba, dawa  na vitabu vya mwongozo  wa matibabu vyenye thamani zaidi ya shilingi milioni 200 vimetolewa na  madaktari kutoka Jamuhuri  ya Watu wa China, wanaofanya kazi   hosptali ya Addalla Mzee, Mkoani.

Kiongozi wa timu ya 29 ya madakitari hao,  Youan Tongzhou alisema  vifaa hivyo vimetolewa ili kusaidia matibabu kwa wananchi wa kisiwa hicho

Akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu wa wilaya Mkoani, alisema wameamua  kutoa msaada huo kwa lengo la kukabiliana na maradhi kwa wagonjwa wanaofika katika hospitali hiyo.

 “Tangu tuanze kufanyakazi hospital Abdalla Mzee ni mwaka sasa, tumeona mambo mengi ambayo yanahitaji kusaidiwa ikiwemo vifaa tiba, hivyo tumejitolea kutokana na mapenzi makubwa tuliyonayo kwa wananchi wa Pemba,” alisema.

Akipokea vifaa hivyo, Mkuu wa wilaya ya Mkoani, Issa Juma Ali, alisema  uwepo wa madaktari hao imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Pemba.

Alimshukuru kiongozi wa timu hiyo kwa kujitolea kwa moyo wa dhati kusaidia na kuwataka wafanyakazi kuwa wazalendo na kuzidisha ushirikiano.

Aidha aliwataka wafanyakazi kuvitunza, kuvithamini na kuvilinda vifaa hivyo ili vidumu kwa muda mrefu. “Mvitunze na mvithamini vifaa vyetu tulivyopatiwa, tujiepushe na vitendo vya udokozi, tukimshika mfanyakazi na vifaa hivi nje ya hospitali kwa matumizi binafsi au kuviuza tutamchukulia hatua,” alisema.