NA ASIA MWALIM
JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja limewashikilia dereva 12 wa gari za mizigo kwa makosa tofauti ya usalama barabarani ikiwemo kuzidisaha mizigo, kubeba mzigo kwa njia ya hatari, kuendesha magari mabovu na kuendesha gari wakiwa wamelewa.
Kamandawa Polisi Mkoa huo, Kamishana Msaidizi (ACP) Awadh Juma Haji, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Mwembemadema Mjini Zanzibar.
Kamanda Awadh alisema madereva hao walikamatwa kati ya tarehe 17 na 18 ya Agosti mwaka huu, katika maeneo mbali mbali ya Mjini Magharibi, wakati jeshi hilo likiwa katika opersheni za usalama barabarani, ili kudhibiti ajali ambazo zinasababishwa na uzembe wa madereva.
Aidha Kamanda alimtaja aliyekamatwa kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa ni Fahmi Ali Abdallah (27) mkaazi wa Bububu, akiwa katika barabara hiyo ambae alikamatwa majira ya saa 1:15 asubuhi akiwa amelewa.
Alifahamisha kuwa dereva huyo alikamatwa wakati akiendesha gari yenye namba za usajili Z.309 GR aina ya ALTEZA na alipopimwa alikutwa na ulevi wa kiwango cha 114.23mlg jambo ambalo ni kinyume na sheria.