NA HUSNA SHEHA
MANISPAAA ya Magharibi ‘A’ Unguja, imeyafungia maduka sita kufanyabiashara zake baada ya kubaini kuuza vyakula vilivyopitwa na muda wa kutumika.
Akizungumza na Zanzibar Leo, huko Ofisini kwake Kianga Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Jamii Afya na Mazingira, Asha Salum Bakari, alisema wameamua kuchukua hatua hiyo, ili wananchi waepuke kuuziwa bidhaa zilizopitwa na muda.
Mkuu huyo alitaja bidhaa zilizokamatwa katika maduka hayo ni pamoja na biskuti, soda za cipy, siagi aina ya Blue band, Cocoa, Marashi, pamoja na maziwa ya Nida.
Hata hivyo, Mkuu huyo aliwataka wananchi watowe taarifa kwa Baraza la Manispaa, ili kuwafichuia watu kama hao na aliwataka wafanyabiashara kufuata sheria inayowataka kuwa na utaratibu mzuri wa kuendesha kazi zao kwa kuhakikisha wanafuata masharti waliyopewa.
Alisema hivi sasa mvua za vuli zimeanza kunyesha na pindipo wafanyabiashara hawatokuwa makini kutunza mazingira kuna hatari ya maradhi ya miripuko kujitokeza na ni vyema wakafuata masharti ya afya.
Alisema operesheni hiyo itaendelea siku hadi siku, ili kuona jamii inabadilika katika kuuza biashara zao maeneo yanayohitajika huku wakizingatia muda wa kutumika.
Pia alisema wamejipanga kutoa elimu kwa njia ya mikutano, redio na Televisheni, ili kuongeza uelewa kwa jamii, huku wakiimaarisha ukaguzi katika shehia 31 za wilaya hiyo.