NA NASRA MANZI
KOCHA Mkuu wa Muembeladu FC, Ramadhan Madundo, ameiomba Serikali kuwekeza katika soka la vijana ili kuongeza hamasa ya mchezo huo nchini.


Akizungumza na Zaspoti hivi karibuni, alisema, ni vyema kuwekwa mikakati mizuri ambayo itakuwa chachu ya kuleta mafanikio na mustakabali bora wa soka ya Zanzibar.


Alisema ikizingatia kwamba Zanzibar imejaaliwa kuwa na vipaji vingi vya vijana kwenye michezo, itakuwa jambo jema kujengewa mazingira yatakayosaidia kuwakuza na kusajiliwa ndani na nje ya Tanzania.


“Tunajivunia vipaji vyetu kwa vijana, lakini na hili la kuwekeza litiliwe mkazo, lengo letu sisi walimu kupata wachezaji imara na kufaidika kwa taifa”, alisema.


Aidha, alisema, kutokana na michezo kumjenga mtu kiakili, kiafya pamoja na kupata upeo katika maisha, vijana hawanabudi kujiepusha kujiingiza katika mazingira yasiofaa ambayo yataharibu malengo waliyojiwekea.