JERUSALEMU,ISRAEL

MAELFU  ya waandamanaji walimiminika katika barabara karibu na makaazi rasmi ya Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika eneo la Kati la Jerusalem wakionesha tena upinzani wao wakati maandamano ya wiki kadhaa dhidi ya kiongozi huyo yakikosa kuonyesha dalili ya kupungua.

Katika kipindi chote cha msimu wa kiangazi, maelfu ya raia wa Israel walikuwa wakifanya maandamano ya kumtaka Netanyahu ajiuzulu huku wakilalamika kuhusu jinsi anavyolishughulikia janga la virusi vya corona na kusema hapaswi kuwa ofisini wakati anapokabiliwa na kesi ya mashitaka ya ufisadi.

Wafanyabiashara ambao biashara zao ziliathirika kutokana na janga la virusi vya corona pia walishiriki katika maandamano ya jana.

Ijapokuwa Netanyahu alijaribu kupuuza maandamano hayo,inaonekana kuongezeka nguvu.

Maandamano hayo dhidi ya Netanyahu ni makubwa zaidi kushuhudiwa nchini Israeli tangu maandamano ya mwaka 2011 yaliyochochewa na kuongezeka kwa gharama ya maisha.