UGONJWA wa corona ambao hadi hivi sasa unaendelea kuyasumbua mataifa mbalimbali ulimwenguni, uliingia barani Afrika mnamo mwezi Machi mwaka 2020.

Barani Afrika ugonjwa huo umeleta athari kubwa na bado athari zake zinaendelea kushuhudiwa hasa ikizingatiwa kuwa bado ugonjwa unaendelea kuyaathiri mataifa mbalimbali ya Afrika.

Hata hivyo, unapotaja nchi iliyoathirika zaidi na ugonjwa huo barani Afrika hapana shaka ni taifa la Afrika Kusini, ambapo pamoja na jitihada kadhaa kuchukuliwa kuudhibiti ugonjwa hao bado kasi ya maambukizi nchini humo ni kubwa.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliofariki kwa ugonjwa wa corona ni pamoja na binti wa aliyekuwa rais wa Afrika Kusini na shujaa wa ukombozi nchini Nelson Mandela, Zindzi Mandela aliyefariki hivi karibuni katika hospitali moja mjini Johannesburg.

Taarifa zimetolewa na msemaji wa chama tawala cha Afrika Kusini, African National Congress (ANC), zilieleza kuwa Zindzi Mandela ambaye mama yake alikuwa mwanaharakati dhidi ya ubaguzi wa rangi, Winnie Madikizela Mandela.

Shirika la utangazaji la taifa SABC, limesema binti huyo wa Mandela mwenye umri wa miaka 59 ambaye alikuwa ni balozi wa Afrika Kusini nchini Denmark amefariki katika hospitali mjini Johannesberg ingawa ugonjwa uliomuuwa haukutajwa.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi hadi Agosti 4 mwaka huu, watu 8,539 wamekwisha fariki dunia, huku idadi ya walioambikizwa ikifikia watu 516,862 na watu 358,037 wameugua na kupona.

Kutokana na hali ya mamabukizi na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo, Afrika Kusini limekuwa taifa nambari moja barani Afrika lililoathirika zaidi na ugonjwa wa corona ikiwemo kupoteza idadi kubwa ya watu.

Kwa takwimu za kiulimwengu Afrika Kusini linakuwa taifa la tano lililoathiriwa zaidi kwa ugonjwa wa corona, likitanguliwa na Marekani, Brazil, India na Urusi.

Watafiti wanahofia idadi hiyo huenda ikwa kubwa zaidi, lakini rais Cyril Ramaphosa amesema idadi ya vifo ni ya uwiano wa chini kabisa duniani.

Afrika kusini inatambulika kuwa na mfumo wa afya imara kabisa barani Afrika lakini pana madai juu ya ufisadi. Rais Ramaphosa amewashutumu watu wanaojitajirisha kutokana na janga la corona.

Pamoja na Afrika Kusini kwa sasa kupitia kwenye ugumu na machungu ya ugonjwa wa corona, lakini ugonjwa huo umekuwa neema kwa mafisadi nchini humo ambao wamekuwa wakijipatia manufaa makubwa kinyume cha sheria.

Ndio maana waswahili wa pwani ya Afrika Mashariki waliwahi kusema kuwa kufa kufaana na pengine wanaonufaika kutokana na ugonjwa huo hata wasingependa kuona ipo siku ugonjwa huo unadhibitiwa kwa sababu maslahi yao yatakatika.

Mamlaka ya kupambana na ufisadi nchini Afrika Kusini ilisema inachunguza madai ya ufisadi katika utoaji wa zabuni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kupambana na janga la corona nchini humo.

Muendesha mashitaka nchini humo ameanza uchunguzi dhidi ya ufisadi uliofanywa na watumishi wa umma, ambapo uchunguzi huo unajiri baada ya kuibuka madududu kwenye kandarasi za ununuzi wa vifaa vya corona.

Mwendesha mashitaka mkuu nchini humo anachunguzwa baadhi ya maofisa kuhusiana na ununuzi wa vifaa vya kuwakinga madaktari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona wanapowashughulikia wagonjwa, katika mkoa wa Gauteng, ambao ndio kitovu cha ukuaji wa uchumi wa Afrika kusini.

Rais Cyril Ramaphosa aliyeingia madarakani akiwaahidi wananchi wa taifa hilo kuwa atapambana na ufisadi baada ya mtangulizi wake Jacob Zuma kuondolewa madarakani na chama chake cha Africa National Congeress – ANC akikabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Ramaphosa aliahidi kwamba serikali yake itawachukulia hatua kali wote wanaotumia njia zisizofuata sheria wakishirikiana na maofisa wa serikali kupora mali ya umma.

“Hatutaruhusu mali ya umma ambayo imepatikana kwa hali ngumu na walipa ushuru, wafadhili na jumuiya ya kimataifa kutoweka kutokana na ufisadi,” alisema Ramaphosa.

Muungano mkubwa wa wafanyakazi nchini Afrika Kusini (COSATU) na ambao unashirikiana sana na chama kinachotawala cha ANC, umesema katika taarifa yake kwamba serikali ya Ramaphosa imechukua hatua za haraka kupambana na madai hayo ya ufisadi.

Muungano huo umetaja ufisadi kuwa tishio kubwa la uchumi wa Afrika Kusini na waliofanya hivyo wamevukwa na imani dhidi ya wananchi wa Afrika Kusini kwa kutaka kutumia janga la corona kujinufaisha.

Mwendesha mashtaka ya umma alisema kwamba ofisi yake inachunguza madai ya ufisadi katika mikoa mitatu, ikiwemo kituo cha karantini kinachosemekana kumilikiwa na ofisa wa serikali, pamoja na ununuzi wa vifaa vya matibabu kutoka mkoa wa Kwa Zulu Natal.

Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance, kimetoa wito kiitishwe kikao cha bunge haraka iwezekanavyo ili kujadili kile ilichokitaja kuwa ‘sherehe ya watu kula’ inayofanywa na watu kutoka chama kinachotawala cha ANC.

Inaripotiwa kwamba kanuni za kisheria katika utoaji wa zabuni katika ununuzi wa vifaa vya matibabu kwa wagonjwa wa corona zilivunjwa na zabuni kutolewa kwa ushirikiano wa watu.

Msemaji wa chama cha ANC hakupatikana kwa simu alipotafutwa na shirika la habari la reuters, ili ajaribu kuelezea kadhia hizo za ufisadi zilizosababisha gumzo kubwa nchini Afrika Kusini.

Msemaji wa rais Cyril Ramaphosa, Khusela Diko na ofisa wa afya wa ngazi ya juu katika mkoa wa Gauteng wamechukua likizo ya dharura wakipishwa uchunguzi wa mwendesha mashitaka.

Taarifa zinaeleza kuwa mume wa Khusela Diko ambaye ni msemaji wa rais, ndiye aliyeshida zabuni ya kununua vifaa vya matibabu katika serikali ya mkoa Gauteng.

Diko na mumewe wamesisitiza kwamba hawajafanya kosa lolote na ofisa huyo wa afya amedai kwamba hakujihusisha na ununuzi wa vifaa hivyo.