MYKONOS, Ugiriki

NAHODHA wa Manchester United, Harry Maguire huenda akafungwa jela kwa miaka mitatu, baada ya kuhusika kwenye vurugu nchini Ugiriki alipokuwa kwenye mapumziko katika kisiwa cha Mykonos.

Inadaiwa kuwa mashabiki kutoka kwa klabu hasidi walimrushia vijembe Maguire na ripoti nyingine zinadai kuwa alighadhabishwa baada ya dada yake Daisy, kushambuliwa na kifaa butu akiwa matembezi usiku.

Kisa hicho kilipelekea kukamatwa kwa mlinzi huyo Ijumaa, Agosti 21 asubuhi, kabla ya kufikishwa kortni.

 Muingereza huyo alikanusha mashtaka dhidi yake huku akihojiwa na viongozi wa mashtaka kwa karibu saa mbili.

Inadaiwa kuwa mashtaka hayo ni pamoja na kufanya vurugu dhidi ya maafisa, utovu wa nidhamu, kujeruhi, matusi na kujaribu kumhonga ofisa mmoja.