SANAA,YEMEN

MAHAKAMA moja nchini Yemen imewahukumu kifo mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman na mrithi wa ufalme wa Imarati, Mohammed bin Zayed, kwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen.

Mahakama Maalumu ya Jinai katika mji wa bandari wa Hudeydah nchini Yemen ilitoa hukumu hiyo dhidi ya watu 16 wakiwemo Bin Salman na Bin Zayed kwa ama kula njama au kutekeleza mauaji ya Saleh al-Samad, aliyekuwa Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen. 

Wengine waliomo kwenye orodha hiyo ya watu waliohusika na mauaji ya al-Samad ni Abd Rabbuh Mansur Hadi,Rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na kukimbilia Saudi Arabia na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Yemen, Ahmed Obeid bin Daghr.

Mkuu huyo wa zamani wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen aliuawa katika shambulizi la anga la Saudia na vibaraka wake katika mji wa Hudeydah, magharibi mwa Yemen mwezi Aprili mwaka 2018.

Mapema mwezi huu pia, Mahakama ya Washington DC ilimtaka Bin Salman na wenzake 13 kufika mahakamani nchini Marekani kujibu tuhuma za kufanya jaribio la kutaka kumuua kigaidi Saad al Jabri, mkuu wa zamani wa Idara ya Intelijensia ya Saudi Arabia aliyekimbilia nchini Canada.

Saudia, Umoja wa Falme za Kiarabu na washirika wao wanaendelea kumwaga damu za Raia wa Yemen tokea mwaka 2015, licha ya malalamiko ya jamii ya kimataifa na wasi wasi wa taasisi mbali mbali za kutetea haki za binadamu duniani.