NA HUSNA SHEHA

MAHAKAMA ya Mkoa Mfenesini, imemnyima dhamana mshitakiwa Khamis Ame Foum (21) mkaazi wa Nungwi Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, anaekabiliwa na tuhuma ya kupatikana na dawa za kulevya aina ya Heroini, zenye uzito wa gramu 1.1238.

Hakimu Faraji Shomari Juma, alimnyima dhamana mshitakiwa huyo kwa madai ya kuwa kiwango  alichopatikana nacho ni kikubwa na hakina dhamana.

“Kutokana na kiwango ulichopatikana nacho ni kikubwa haiwezekani kupewa dhamana”, alisema Hakimu huyo.

Awali mshitakiwa alisomewa shitaka lake na Mwendesha mashitaka wakili wa Serikali Hamadi Zidi Kheir, alidai kuwa Juni 22 mwaka huu majira ya saa 8:39 mchana huko Nungwi kwa Mpapai, mshitakiwa huyo bila ya halali alipatikana na kete 62 za dawa za kulevya.

Upande huo wa mashitaka ulidai kuwa, kitendo cha kupatikana na dawa za kulevya ni kosa, kinyume na kifungu cha 16 (1) (a) cha sheria namba 9 ya mwaka 2009, kama ilivyorekebishwa na kifungu cha 11 (a) cha sheria namba 12 ya mwaka 2011 sheria ya Zanzibar.   

Baada ya kusomewa shitaka hilo mshitakiwa alikataa kosa na kuiomba mahakama impatie dhamana, ombi ambalo halikukubalika kwa pande zote mbili.

Hata hivyo alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umeshakamilika na kuiomba mahakama impangie tarehe nyengine kwa kusikiliza ushahidi.

Mshitakiwa Khamis Ame Foum, amepelekwa rumande na atafikishwa tena mahakamani hapo Agosti 10 mwaka huu kwa kusikilizwa mashahidi na mashahidi waitwe.