NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda  amesema kuwa alitamani katika uongozi wake angepima wananchi saratani ya tezi dume kaya kwa kaya, lakini alishindwa kwasababu  ya kukosekana kwa muda.

Hayo aliyasema jana wakati akikabidhi ofisi kwa Mkuu wa Mkoa mpya, Abubakar Kunenge aliyeteuliwa na Rais John Magufuli hivi karibuni, ambapo alisema  yapo mambo mengi ambayo alitamani kuyatekeleza katika nafasi yake.

Alisema kuwa moyo wake unaweza ukajuta na nakujisikia vibaya katika upimaji wa tezi dume kaya kwa kaya, nilitamani sana kulifanya lakini kwasababu ya ratiba tulikwama.

Aidha alisema kuwa  saratani yatezi dume inatesa watu huku wengine wakiona aibu kwenda hospitali kupima wengine wakifikiri ni kwa ajili ya wanaume tu.

Alimshukuru Rais Magufuli kwa kuitii sauti ya Mungu na kumuamini katikati ya wengi wasio muamini  na kumniteua kuwa Mkuu wa Mkoa huo.

Alisema kazi ya uteuzi si rahisi lakini Rais aliamini katika vijana huku akiwa kijana wa kwanza kupewa majukumu kwenye Mkoa mkubwa na kuacha alama itakayodumu.

“Lakini Rais aliziba masikio akaendelea kuniamini na hatimaye tarehe 15  nimeondoka mwenyewe ikiwa ni ishara ya kukubali kazi niliyoifanya na kuamini imefika wakati uende kwenye majukumu mengine,”alisema.

Alisema amepita kwenye mambo mengi lakini vita ya dawa za kulevya haiwezi sahau huku akibainisha kuwa kila mtu alipiga kelele ambapo Rais hakuyumbishwa na msimamo huo.

Aidha alisema kuwa  Rais alimuamini na kuamini anachokifanya ni kwa faida ya watanzania na kuibuka kidedea kwa ushindi dhidi ya mapambano ya dawa za kulevya.

Makonda alisema Rais Magaufuli ametoa nafasi ya kusimamia kazi kwani hapo awali Jiji hilo halikuwa na utulivu, Amani lakini walishirikiana na kuwa na Amani kwa sasa.

Alisema nchi kama ingechelewa kumpata Rais Magufuli basin chi ingekuwa nyuma kimaendeleo huku akibainisha kuwa Rais anathubutu, kuamini kwenye kazi na si majungu.

Makonda alimuomba Mkuu wa Mkoa, kumkabidhi barabara Cardinal Pengo ambayo aliwahi kutamka kumkabidhi pamoja na Mbwana Samatta kwa kuwaenzi kutokana na huduma wanazotoa.

Alisema anaamini amemaliza mwendo vizuri huku akibainisha kuwa kama binadamu anaweza kuwa na mapungufu yake ambayo yanawezekana yametokana na kutokuwepo kwa taarifa sahihi ya maamuzi yaliyoamuliwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huo, Kunenge alisema walikuwa wakifanya kazi pamoja wakati huo akiwa Katibu Tawala wa Mkoa huo (RAS) hivyo ataendeleza yote waliyokuwa wakiyafanya pamoja na kushauriana natakayofaa.