NA MARYAM SALUM, PEMBA

ILITAJWA enzi hizo kuwa, malezi ya pamoja ni njia moja wapo iliyoweza kuisaidia jamii katika kuweza kupambana na majanga mbali mbali kwa watoto wao.

Malezi hayo, yalisaidia kwa hali moja ama nyengine katika kutatua shida nyingi za kijamii, ikiwemo hata mlo wa siku baina ya familia moja na nyingine.   

Wazee wa zamani walikuwa na ushirikiano wa dhati katika malezi ya pamoja kwa watoto, ili watoto wakue kwenye misingi bora na ya historia tena yenye heshima.

Ndio maana leo nakuja mbele yenu, kusema kuwa malezi ya pamoja kama yakirejeshwa yanaweza kuwa mwafaka kumaliza matatizo kadhaa hususan suala la udhalilishaji kwa wanawake na watoto wetu.

Kutokana na hali hiyo watoto walikuwa wakiishi kwenye misingi bora ya kiheshima, walikuwa ni wenye tabia njema kwa wazazi wao, na wa wenzao pamoja na kupeana heshima kwa watoto wenye rika moja.

Lakini kutokana na kuondoka kwa malezi hayo ya pamoja vitimbi vingi, mikasa kadhaa wakadhaa vimekuwa vikijitokea ndani ya jamii zetu zilizotuzunguka.

Kwanini tusiwe tayari kuyarejesha malezi ya pamoja, ili ule utamaduni uliokuwepo zama za mababu na mabibi zetu ukaendelea kuwa dawa kwa vitendo hivi.

Jamii sasa imezungukwa na majanga likiwemo janga zito la udhalilishaji kwa wanawake na watoto, hii inatokana na sababu kadhaa, lakini sababu ya msingi ni kuondoka kwa malezi ya pamoja.  

Kuondokana na utamaduni huo wa malezi ya pamoja, inaonekana ndio chanzo kikuu kwa wanaofanya unyama huo, ambapo zamani walikuwa wafalme, lakini sasa hivi wamekuwa wavunjifu wakubwa wa amani kwa watoto.   

Hivi nikuulize wewe baba zima mwenye miaka hamsini hadi tisiini, huoni huna huruma, huoni vibaya kuthubutu kunyanyua viungo vyako kumfanyia mtoto vitendo vya ukatili.

Hebu kuweni na aibu, hawa watoto ambao mnawafanyia vitendo vya udhalilishaji oneni kama kwamba ni sawa na watoto wenu ambao mliwazaa.

Kimtazamo ulivyo ongezeka kwa matendo ya udhalilishaji ni kutokana na uondokaji wa malezi ya pamoja, ambayo yalikuwepo hapo zamani.

Kama hatuoni, basi tunasikia jinsi matendo yanavyozidi kuongezeka ndani ya jamii, kwanini sasa tusijenge imani, tukarejesha malezi ya zamani kuondosha hii kadhia, ili watoto wabaki katika mazingira salama.