BAMAKO,MALI

VIONGOZI wa kijeshi ambao wamechukua madaraka hivi karibuni nchini Mali wanataka kipindi cha mpito nchini humo kidumu miaka mitatu chini ya uongozi wa mwanajeshi.

Hayo yalibainika katika mkutano baina ya baraza la kijeshi na wapatanishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ambao ulifanyika katika mji mkuu, Bamako .

Wawakilishi wa ECOWAS waliwasili Bamako, Mali siku ya Jumamosi katika mazungumzo ambayo yalilenga kumrejesha madaraknai Rais Ibrahim Boubacar Keita ambaye alipinduliwa jumanne iliyopita.

Wajumbe wa ECOWAS, wakiongozwa na Rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan, walifanya mazungumzo marefu na viongozi wa mapinduzi ya kijeshi walioongozwa na Kanali Assimi Goita.

Jonathan alisema baada ya mazungumzo ya masaa tisa walifikia mapatano kuhusu baadhi ya masuala.

Ujumbe huo wa ECOWAS unaendeleza mazungumzo na wanajeshi kuhusu hatima ya Mali.

Naye Msemaji wa baraza la kijeshi Kanali Ismael Wague alisema wamefikia mapatano kuhusu baadhi ya masuala na mazugumzo yanaendelea.

Mapinduzi ya kijeshi nchini Mali yalitokea Jumanne iliyopita ambapo Rais Ibrahim Boubacar Keita na Waziri Mkuu wake, Boubou Cissé walitiwa mbaroni na wanajeshi waasi. Masaa machache baada ya kukamatwa, Rais Keita alijitokeza katika televisheni ya taifa na kutangaza kujiuzulu huku akisisitiza hataki kubakia kwake madarakani kuwe chanzo cha umwagikaji damu nchini humo.