NA MARYAM HASSAN
MALUMBANO ya kisheria baina ya Wakili wa serikali na wa utetezi yaliyozuka katika mahakama ya mkoa Vuga, yamepelekea kesi ya mshitakiwa Maico God Sendeki mkaazi wa Ziwatuwe kuahirishwa.
Mabishano hayo yamekuja baada ya wakili anaemuwakisha mshitakiwa huyo anaekabiliwa na makosa mawili kubaka na kutorosha kuiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa madai kuwa wakili husika wa mshitakiwa huyo yupo Tanzania bara kikazi.
Wakili wa utetezi Lydya Mhando aliyasema hayo mbele ya Hakimu Valentina Katema wa mahakama ya mkoa Vuga, huku upande wa wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka alikuwa ni Ahmed Mohammed.
Lydya amesema, kwa upande wake hatoweza kusikiliza shahidi aliyefikishwa mahakamani hapo, kwa sababu si mhusika na badala yake ameiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo na kupangwa tarehe nyengine.
Lakini hali ilikuwa tofauti kwa wakili wa serikali, ambae alisema hoja alizotoa wakili wa mshitakiwa si za msingi na kuiomba mahakama kuzitupilia mbali.
Alisema upande wao wamepokea shahidi mmoja na yupo tayari kumsikiliza, huku akiitaka Mahakama kuzingatia kuwa kwa kipindi cha miezo mitatu walishindwa kusikiliza mashahidi, kwa sababu ya kuzuka kwa maradhi ya Corona hapa nchini.
Hivyo aliitaka mahakama kuzingatia muda huo na badala yake amsikilize shahidi huyo kwa kuwa amefika mahakamani ili kesi hiyo imalizike haraka.
“Tunaiachia mahakama lakini sababu alizotoa wakili si za msingi kwa sababu zinasababisha kuzorota kwa kesi hii”, alisema Ahmed.
Baada ya mabishano hayo Hakimu Valentina kwa mamlaka aliyopewa aliahirisha shahuri hilo hadi Agosti 12 mwaka huu kesi hiyo itaposilizwa ushahidi.
Pia alimuonya shahidi huyo na kumtaka tarehe hiyo kufika mahakamani na asipofika hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka kwa mshitakiwa huyo, alidaiwa kutenda kosa la kutorosha Julai 12 mwaka jana majira ya saa 1:00 za asubuhi huko Ziwatuwe mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Mshitakiwa alidaiwa kumtorosha mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13 ambaye yupo chini ya uangalizi wa wazazi wake, kutoka nyumbani kwao Ziwatuwe na kumpeleka kwenye chumba cha mshitakiwa huyo huko huko Ziwatuwe.
Ilidaiwa kuwa baada ya kumtorosha alimuingilia kimwili msichana huyo (Jina linahifadhiwa na gazeti hili) jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria.