NA MARYAM HASSAN
MALUMBANO ya kisheria baina ya Wakili wa serikali na wa utetezi yaliyozuka katika mahakama ya mkoa Vuga, yamepelekea kesi ya mshitakiwa Maico God Sendeki mkaazi wa Ziwatuwe kuahirishwa.
Mabishano hayo yamekuja baada ya wakili anaemuwakisha mshitakiwa huyo anaekabiliwa na makosa mawili kubaka na kutorosha kuiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa madai kuwa wakili husika wa mshitakiwa huyo yupo Tanzania bara kikazi.
Wakili wa utetezi Lydya Mhando aliyasema hayo mbele ya Hakimu Valentina Katema wa mahakama ya mkoa Vuga, huku upande wa wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka alikuwa ni Ahmed Mohammed.
Lydya amesema, kwa upande wake hatoweza kusikiliza shahidi aliyefikishwa mahakamani hapo, kwa sababu si mhusika na badala yake ameiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo na kupangwa tarehe nyengine.
Lakini hali ilikuwa tofauti kwa wakili wa serikali, ambae alisema hoja alizotoa wakili wa mshitakiwa si za msingi na kuiomba mahakama kuzitupilia mbali.
Alisema upande wao wamepokea shahidi mmoja na yupo tayari kumsikiliza, huku akiitaka Mahakama kuzingatia kuwa kwa kipindi cha miezo mitatu walishindwa kusikiliza mashahidi, kwa sababu ya kuzuka kwa maradhi ya Corona hapa nchini.
Hivyo aliitaka mahakama kuzingatia muda huo na badala yake amsikilize shahidi huyo kwa kuwa amefika mahakamani ili kesi hiyo imalizike haraka.
“Tunaiachia mahakama lakini sababu alizotoa wakili si za msingi kwa sababu zinasababisha kuzorota kwa kesi hii”, alisema Ahmed.