ABUJA,NIGERIA
WANAMGAMBO wenye itikadi kali wamewateka nyara mamia ya watu kwenye mji wa kaskazini mashariki ya Nigeria, ambako raia walikuwa wakirejea nyumbani baada ya kukimbia makaazi yao.
Wanamgambo wa kundi liitwalo ISWAP walivamia eneo la Kukawa kwenye mkoa wa ziwa Chad na kuwakamata watu waliokuwa wakirejea nyumbani baada ya kuishi kwenye kambi za wasio na makaazi kwa miaka miwili.
Kwa miaka kadhaa sasa Nigeria ilikuwa ikilengwa na wapiganaji wa ISWAP kwa mashambulizi ya mara kwa mara na utekaji nyara wa raia ikiwa ni moja ya mbinu zinazotumiwa na makundi ya itakadi kali.
Mwaka 2018 kundi hilo liliwateka zaidi ya wanafunzi wa kike 100 kutoka kwenye mabweni yao tukio ambalo lilirejesha kumbukumbu ya tukio kama hilo la kutekwa wanafunzi wa kike 300 kwenye mji wa Chibok katika jimbo la Borno.