NA LAYLAT KHALFAN
BARAZA la Manispaa Magharibi ‘A’, kupitia kitengo chake cha Kilimo, Maliasili na Mazingira, kimesema kinatarajia kuvisafisha visima vyote vilivyopo Bumbwisudi wilayani humo, ili kuepusha kuungua pampu mara kwa mara zinazosambaza maji katika kilimo cha umwagiliaji mpunga.
Mkurugenzi Kilimo, Maliasili na Mazingira wa Baraza hilo, Hassan Juma Salum, aliyasema hayo ofisini kwake Kianga wakati alipokuwa akizungumza na Mwandishi wa habari wa gazeti hili.
Alisema imebainika kuwa bomba za visima hivyo ni vya zamani ambazo zina kutu na nyengine zinatundu hali inayosababisha mota kunyonya uchafu na kuharibika kwa urahisi.
“Hii miundombinu ya umwagiliaji maji mengi yao ni chakavu kwani tumeirithi kutoka Wizara ya Kilimo lakini hata hivyo nia yetu ni kuikarabati upya na kuongeza mengine ili kilimo chetu kiwe na tija kwa kuweza kujitegemea wenyewe”, alisema.
Aidha, Hassan alisema mpango huo wa kusafisha visima upo mbioni na unatarijia kuanza muda wowote kuanzia sasa ambao unalenga kuzuia pampu kutoharibika mara kwa mara na wakulima kuweza kufaidika katika kilimo chao cha umwaigiliaji.
Alifahamisha kuwa, mara nyingi wanapokea kesi za wakulima kutokana na visima hivyo kutosambaza maji kikawaida na kusababisha kuduma kwa zao lao.
Alieleza kuwa visima vyote ni 16 kati ya hivyo vitatu havifanyi kazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuungua huku wakiwa na malengo ya kuzalisha hekta 300 badala ya hekta 200 wanazovuna.