NA TATU MAKAME
BARAZA la Manispaa Mjini limeanza zoezi la kuwaondosha wafanyabiashara wadogowadogo wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa barabara na maeneo ya wazi katika eneo la Darajani ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Hatua hiyo imelenga kupunguza msongamano wa watu katika maeneo hayo lakini pia kuwarejesha katika maeneo yaliyotengwa kwa shughuli hizo yakiwemo la Saateni na Kijangwani.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Malindi mjini Unguja, Ofisa habari wa baraza hilo Seif Ali Seif, alisema lengo jengine ni kuweka mazingira mazuri katika mjini wa Zanzibar.
Alisema wafanyabiashara hao walipangiwa kufanya shughuli zao katika maeneo hayo, lakini wengi wao wanaendesha biashara maeneo ya wazi na pembezoni mwa barabara hali inayopelekea kuchafua mazingira.
Alieleza kuwa hali hiyo imekuwa ikileta taswira mbaya ya mji na kupelekea kutojuilikana maeneo maalum ya biashara.
Alisema zoezi hilo ni kutekeleza agizo lililotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein wakati alipokutana na uongozi wa baraza hilo kuwaondoa wafanyabiashara hao wakati wa kikao cha mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo karibuni.
Alieleza kuwa baada ya kutolewa kwa maagizo hayo, baraza hilo limeanza kutekeleza agizo hilo la kuwaondosha wafanyabiashara wanaofanya biashara maeneo hayo.
Aidha alisema mfanyabiashara atakaekaidi agizo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kulipishwa faini.
Akizungumzia changamoto iliyojitokeza kwa baraza la manispaa kuondoka maeneo waliyopangiwa kupungua kwa ukusanyaji wa mapato na kupelekea hasara kwa serikali.
Aliwataka wafanyabiashara kufuata maelekezo wanayopatiwa na baraza hilo kwa lengo la kuuweka mji katika hali ya usafi na kuwa wenye kuvutia.