NA MWANTANGA AME
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, wiki za karibuni alifanya mazungumzo na uongozi wa Mkoa wa Mijini Magharibi pamoja na Manispaa yake na kuutaka kuhakikisha mji wa Zanzibar unakuwa safi kwani tayari hivi sasa unahadhi ya Jiji.
Dk. Shein aliyasema hayo huko Ikulu Jijini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ wakati ilipowasilisha Taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2019/2020 na Mpango Kazi wa mwaka 2020/2021.
Alieleza kuwa kuna haja ya kuweka mikakati maalum katika kuhakikisha mji wa Zanzibar unaendelea kuvutia na kufikia malengo laye ya kuufanya kuwa Jiji kutokana na sifa zote ulizonazo.
Rais Dk. Shein alisema kuwa ipo haja kwa uongozi wa Mkoa kuangalia suala zima la usafi hasa katika masoko na barabarani, kwani wengi ya wafanyabiashara wamevamia maeneo hayo na hatimae kuufanya mji kutokuwa msafi sambamba na kuepuka ajali ambazo zinaweza kutokea kutokana na kufanya biashaara maeneo ya barabara.
Pia, Rais Dk. Shein alieleza haja ya uongozi wa Mkoa huo kufanya kazi kiserikali kwa kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizokuwepo katika kuhakikisha biashara zote zinafaywa kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo.
Alieleza kuwa licha ya Serikali kubuni mpango wa masoko mapya, lakini hata hivyo katika eneo la soko la Mwanakwerekwe bado pamekuwa na msongamano mkubwa wa wafanyabishara ambao hufanya shughuli zao hizo pembezoni mwa barabara.
Alieleza haja ya kuandaa utaratibu maalum wa kuwaweka wafanyabiashara katika mazingira mazuri pale wanapowaondoa kutoka eneo moja kwenda eneo jengine kwa ajili ya kufanya biashara zao.
Kauli hii ya Dk. Shein, inaenda sambamba na ule usemi wa ‘Lisemwalo lipo, kama halipo laja’ lakini huo ndio ukweli kama Mji kuwa safi ni moja ya kivutio kizuri na uchafu ni kero kubwa ambapo hivi sasa inaonekana katika maeneo mbali mbali hairidhishi.
Ikumbukwe kwamba Zanzibar ni nchi yenye historia kubwa na vivutio vingi vya kitalii ambavyo vimekuwa vikiingizia fedha nyingi za kigeni na hivyo kuinua uchumi wake na hali za wananchi kwa jumla.
Miongoni mwa vivutio hivyo, ni urithi wa Mji Mkongwe, magofu ya kihistoria yaliyoenea kila pembe Unguja na Pemba, fukwe za kuvutia, mashamba ya viungo, na zaidi akhlaki za watu wake ambao wanasifika kwa ukarimu na tamaduni zao.
Lakini pamoja na sifa zote nzuri ambazo Zanzibar inazo, bado tatizo la uchafu wa mji ni jambo linalotia doa taswira hiyo njema kwa nchi yetu.
Na hili ndilo linalosababisha mripuko wa maradhi mbalimbali ikiwemo kipindupindu ambacho mara kadhaa kimekuwa kikileta athari kubwa huku serikali ikilazimika kupiga marufuku baadhi ya biashara za vyakula na karamu.
Pamoja na elimu yote inayotolewa kila siku na mamlaka zinazohusika na maendeleo ya miji juu ya umuhimu wa kuiweka safi, bado miji na mitaa yetu iko katika hali ya uchafu unaoiweka nchi katika ramani mbaya.
Licha ya jitihada za mabaraza ya manispaa, bado mitaa yetu mijini na ng’ambo inatia jelezi kuiona kwani taka zinaachwa zikizagaa barabarani na vichochoroni na kuzalisha nzi ambao ni hatari kwa afya za wakaazi na wageni wafikao hapa.
Lililo baya na la aibu zaidi, ni kwamba sisi ni binadamu ambao kimsingi tunatakiwa tufahamu maana na umuhimu wa usafi na tusiwe watu wa kufundishwa na kuhimizwa tu juu ya jambo hilo.
Hatuoni mantiki ya watu wazima kuwa kila siku wanakumbushwa kuweka mazingira safi, lakini Rais wetu Dk. Ali Mohamed Shein hajachoka kutuhimiza kuhusu usafi.
Ingawa anatukumbusha lakini nafikiri tukubali anaeambiwa husikia kwani haipendezi Rais wa Nchi kila siku awe anahimiza usafi wakati kukiwa na watu walipewa mamlaka kubwa kusimamia suala hilo wapo na wanachukua mishahara mikubwa kwa ajili ya kuifanyakazi hiyo huku wengine wakikusanya mapato kila kona ya Mji.
Nafikiri inapaswa kubadilika kwa kuona usafi ni jambo ambalo mtu mwenye akili timamu na maarifa ya kiutu uzima, anapaswa kulifahamu na kulifanya kuwa sehemu ya utamaduni wa maisha yake ya kila siku.
Hivi kweli watu wazima ambao wanajua madhara ya uchafu katika baadhi ya mitaa na maeneo mbalimbali ya miji yetu kuwekwa mabango yanayoandikwa matangazo ya kukataza watu kutupa taka, au kwenda haja ndogo?
Kwa nini mtu mzima na akili zako, utoke nyumbani kwako na kipolo cha taka na kwenda kuzitupa kwenye mtaro wa maji machafu, pembezoni mwa nyumba ya mtu mwengine, au wewe unaeishi ghorofani huoni vibaya kurusha taka, ‘pampers’, au maji machafu kutoka juu kwa kupitia varanda?
Tunapofanya mambo mengine, lazima tupime athari zake, na pia tujiulize iwapo mtu mwengine atatufanyia sisi tutafurahi?
Ni vyema katika hali ya kawaida, wazazi tunapaswa kuwafundisha watoto wetu umuhimu wa usafi, lakini kinyume chake, sisi tumekuwa watu wa kufundishwa na mabaraza ya miji, kwani ndio wachafuzi wakubwa wa mazingira tukiwa nje ya nyumba zetu.
Haitoshi kwetu kuwa watanashati na warembo kwa mavazi mazuri, mapambo kedekede, vipodozi, kuvaa nywele za bandia na kadhalika, lakini miji yetu tukaiacha ikinuka kwa harufu mbaya na uozo.
Tuhitimishe kwa kutoa ushauri kwa wananchi tubadilike na tuachane na utamaduni wa kukumbatia uchafu, tuisafishe na kuitunza miji yetu, kwani hilo ni jukumu la kila mmoja wetu na sio manispaa na halmashauri pekee.
Haitapendeza kuona Rais ajaye nae arudie kauli hii ya kuhimiza usafi kufanyika wakati waliopewa kazi ya kusimamia kazi hiyo wapo na ni vyema wakubali kuifanya kazi zao bila ya kusukumwa.
Nalisema hili kutokana na kinachoonekana wazi kuwa Mji unakuwa mchafu kutokana na baadhi ya watendaji kukataa kusimamia suala hili na ndio maana leo hii huwa si jambo la ajabu kuona taka zimejaa katika makontena na kutapakaa chini kwa siku tatu hadi nne bila ya kuondolewa kisa ni gari hakuna ama gari hazina mafuta.
Kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa linalohitajika kufanywa hivi sasa kuikataa hali hiyo na taasisi hiyo ije na mfumo mpya wa kuufanyia usafi wa Mji badala ya ule uliozoeleka wa kutumia vifaa vya zamani badala ya kisasa.
Hivyo basi ipo haja ya taasisi hii kuona inajipanga kwa vile tayari wameshaona mahitaji yakoje basi iwape nafasi kubadilika kwani Mji ni usafi sio uchafu.