NA TATU MAKAME

BARAZA la Manispaa Mjini, limefanya zoezi la bomoa bomoa ya kuondoa vibanda vya vya biashara vilivyojengwa pembezoni mwa barabara za njia za Mjini Unguja.

Zozei hilo lilisimamiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi na Uendelezaji Ujenzi (DCU), Mohamed Habibu Mohamed, kwa kuondoa vibanda vya wafanyabiashara ndogo ndogo katika maeneo mbali mbali karibu na barabara, ikiwa ni hatua ya kutekeleza agizo la serikali.

Akizungumza na Waandishi wa Habari huko Mnara wa Kumbukumbu Kisonge Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, mara baada ya zoezi hilo kufanyika, Mwenyekiti huyo, alisema wameamua kuviondoa vibanda hivyo baada ya kubaini baadhi ya watu wamejenga maeneo hayo bila ya kufuata sheria kwa vile hawakuwa na vibali kujenga maduka hayo.

Alisema wapo wananchi ambao walijenga maeneo ya wazi bila kupatiwa vibali vya ujenzi, hali inayosababisha usumbufu pale serikali inapoamua kuyatumia maeneo hayo kwa harakati nyengine.