NA ASIA MWALIM

BARAZA la Manispaa Wilaya ya Magharibi B Unguja, limesema linaendelea kufanya usafi wilaya hiyo kama ilivyo kuwa awali ili kuhakikisha linaenda sambamba na utekelezajaji wa agizo la Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein.

Mkurugenzi Msaidizi wa Miundo Mbinu ya Kiuchumi na Kijamii, Haji Bakar Mshinga, aliyasema hayo alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Mombasa Zanzibar.

Alisema baraza hilo limekuwa na kawaida ya kufanya shughuli zake za usafi kila siku kwa maeneo ya shehia 34 za wilaya hiyo, kwa siku sita kila wiki, hali ambayo inapelekea kungarisha mji wa Zanzibar.

Mkurugenzi huyo alisema kufuatia agizo hilo la kuhakikisha mji wa Zanzibar unakuwa safi, limeweza kushajihisha zaidi wafanyakazi wao kuendelea kufanya kazi zao kwa bidii kwenye maeneo mbali mbali ikiwemo soko la Mwanakwerekwe.